Na Salum Vuai
JUMUIYA ya Wewekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI), imeeleza kuridhishwa na namna Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar, zinavyochukua hatua kuhakikisha sekta hiyo inaimarika zaidi na kuchangia pato la taifa.
Akizungumza katika hafla maalumu ya chakula cha usiku iliyojumuisha wanachama wa ZATI kwenye hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini, Mkurugenzi Mtendaji wa jumuiya hiyo Pamela Matthew, alisema ushirikiano wa serikali unachangia sana kuongezeka kwa watalii wanaokuja nchini.
Pamela alikumbusha ujumbe wa Rais wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete alioutoa kwenye 'Swahili International Travel Expo' jijini Dar es Salaam mapema mwezi huu, ambapo Rais alisema, jitihada ziongezewe maradufu kuwezesha mazingira ya sekta binafsi na wadau wengine kuchangia zaidi ukuaji wa utalii.
Akimnukuu Rais Kikwete, Mkurugenzi huyo alisema iko haja ya kufanya kazi ya ziada na nzuri kulingana na hali ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii, utoaji viza, kuweka uwiano wa kodi na ada, kuweka bei za ushindani na kuimarisha huduma kwa watalii ili wafurahie ziara zao na kujua thamani ya fedha zao.
Pamoja na mambo mengine, Pamela alisema suala la usalama katika sekta ya utalii litabaki kuwa ajenda kuu.
Alieleza shukurani zake kuwa, serikali kujidhatiti katika kuimarisha sekta ya utalii, na kwamba agizo lake la kutaka wadau wabebe dhamana na kufanya kazi kwa pamoja kuelekea lengo la
utalii kwa wote, linatekelezwa.
"Ujumbe huu wa Mhe. Rais, unaendana na mikakati ya jumuiya yetu, ambapo uongozi na wanachama wetu wote wanafanya kazi kubwa kuhakikisha utalii unaleta tija kwa umma wa Zanzibar na
Tanzania kwa jumla," alieleza.
Alifahamisha kuwa, takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii wa moja kwa moja waliofika Zanzibar mwaka 2013, ilifikia
181,000 kiwango ambacho ni kikubwa.
Aidha alisema inakadiriwa kuwa wageni wengine 250,000 waliingia visiwani humu kutokea Tanzania Bara wakiwa katika mapumziko, ambapo kwa ujumla idadi hiyo inafanya watalii
waliofika mwaka jana kufikia 400,000.
Pamela alisema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu kadiri sekta hiyo inavyozidi kuimarika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ZATI Abdulsamad Said, alisema jumuiya hiyo imepata faraja kubwa kutokana na jitihada za jeshi la polisi kudhibiti wimbi la vitendo vya kihalifu dhidi ya
watalii.
Alisema kuongeza nguvu za ziada kwa polisi jamii katika ukanda wa utalii, sambamba na jeshi lenyewe, kumesaidia sana kuuweka ukanda huo katika hali ya usalama.
Kutokana na mafanikio hayo, ZATI imelitunuku jeshi la Polisi
Tanzania cheti kwa kutambua ushirikiano na mchango linaotoa katika kulinda usalama wa hoteli na watalii.
Cheti hicho kilipokelewa na Kamishna wa polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame kwa niaba ya jeshi hilo.
Cheti kama hicho pia, kilitolewa kwa Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Salum Nassor.
Mapema, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke, aliyealikwa katika hafla hiyo aliisifu Zanzibar kupitia Kamsheni ya Utalii, jinsi inavyojitangaza kimataifa na kuwavutia watalii wengi kutoka nchi za nje ikiwemo Ujerumani.
Alisema kwa kutumia maonesho ya kimataifa ya utalii yanayofanyika kila mwaka jijini Berlin, visiwa vya Zanzibar vimezidi kung'ara kutokana na kutangaza vivutio vingi maeneo ya kihistoria yaliyopo nchini.
Balozi huyo alisema, kutokana na sifa hizo, ndio maana nchi yake inashika nafasi ya pili kwa kuleta watalii wengi hapa nchini, ikitanguliwa na Italia.
Balozi Kochanke aliahidi kusaidia juhudi hizo kwa kuzidi kuitangaza Zanzibar nchini kwake, ili kuvutia watalii zaidi na hivyo kuimarisha juu uchumi wa nchi hii.