Na Mwandishi wetu
Waziri Ujenzi, Ardhi, Makazi Maji na Nishati, Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban, amesema watu waliopewa nyumba za maendeleo na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume, katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, hawatahamishwa, lakini watakapofariki familia zao zitalazimika kuzilipia kodi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mswada wa sheria ya kuanzisha Shirika la Nyumba katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi jana, alisema familia hizo zitapewa mikataba ya kuzilipia nyumba hizo.
Aidha alisema, wale ambao walivunjiwa nyumba zao kupisha ujenzi wa nyumba hizo wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya kwanza na kulipwa fidia hawataguswa badala yake wapewa hati za kumiliki nyumba hizo kwa sababu ni zao.
Mapema Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mwadini Makame, alisema lengo la kuanzishwa shirika hilo ni kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora.
Hata hivyo, Wawakilishi waliitaka wizara hiyo kuhakikisha shirika hilo linawezeshwa ili kuondoa uwezekano wa kufanya kama ilivyotokea kwa mashirika mengine.
Wajumbe wa Baraza hilo waliupitisha mswada huo kuwa sheria na sasa unasubiri kusainiwa na rais ili kuanza kutumika.