Na Mwandishi wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaachia huru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Michael Petro Mwanda na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, James Andilile, kusubiri ufafanuzi wa Bunge kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Awali, juzi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, ilikutana kujadili suala hilo baada ya viongozi hao kukamatwa.
Kuachiwa kwao kunatokana na kutokuwepo mlalamikaji aliefungua jalada na kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi hao.
Aidha, maofisa wawili wa sekretarieti ya bunge waliitwa polisi kutoa ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo wakiwemo pia mawakili wa watuhumiwa.
Pia iligundulika katika sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge sura ya 296 kifungu 12 (3) kinaonesha kwamba Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali alitakiwa kwanza apendekeze kwa Spika wa bunge juu ya jambo lolote aliloliona kama ni kosa.
Na Spika akiridhia kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa kwake na Mwenyekiti wa kamati ya bunge, ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa.
Katika kikao na jopo la wanasheria iligundulika kwamba katika sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge, agizo la kukamatwa watu hao lililotolewa na Mwenyekiti wa kamati ya bunge lakini halikuzingatia taratibu hali iliyosababisha polisi kuwaachia huru.