Na Mwandishi wetu
Aliyekuwa mweka hazina wa Bunge la SADC, Said Seleman Jaffo, ameutaka uongozi mpya wa Bunge hilo (SADC PF) kuendeleza mazuri yaliyoanchwa na uongozi unaomaliza muda ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi bora ya fedha.
Alisema hayo mjini Victoria Falls alipokuwa akisomo taarifa ya mapato na matumizi ya bunge hilo kabla ya kukabidhi madaraka yake kwa uongozi mpya uliochaguliwa Novemba 2 mwaka huu.
Alisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, aliweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi ya fedha kwa kuanzisha mfumo maalumu uliosaidia kuhakikisha matumizi ya fedha ndani ya bunge hilo yanakuwa ya wazi na yanadhibitiwa.
“Mfumo huu umetusaidia kuleta uwajibikaji ndani ya bunge hili na hasa katika kuhakikisha matumizi ya fedha yote ndani ya bunge hayaidhinishwi na sekretariati pekee,bali Rais wa Bunge hili, Mweka hazina pamoja kamati tendaji wanapata taarifa za matumizi ya fedha kupitia mtandao jambo ambalo si rahisi kwa mtu mmoja kufuja fedha kirahisi kwa kwa kuwa kila kitu kipo katika mtandao,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miezi sita baada ya uanzishwaji wa mfumo huo, bunge hilo limeweza kufanikiwa kuondoa mapungufu yote yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara kama vile upungufu wa fedha na kushindwa kufikia malengo kutokana na ukosefu wa fedha.
“Napenda kuwafahamisha kuwa hadi kufikia mwezi Machi, 2014, taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Bunge hili zilikuwa zinaonesha kuwa tuna upungufu wa fedha, lakini hivi ninavyowaambia mwezi, kasoro hizo hamna tena bali tuna fedha zaidi ndani ya bajeti yetu ambazo ni zaidi ya dola 824,000,” alisema.
Akizungumza nje ya ukumbi baada ya kuwasilisha ripoti hiyo na kumkabidhi mweka hazina mpya mikoba ambaye ni Gary Nkombo kutoka Zambia, Jaffo alisema uanzishwaji wa mfumo huo sio tu umelisaida bunge hilo bali umeipa heshima Tanzania kwa kuwa utaratibu huo ni mpya na umeonesha mafanikio.
Alisema zamani viongozi walikuwa hawana mawasiliano ya moja kwa moja ya nini kinafanyika kuhusu fedha za bunge lakini baada ya kuazishwa mfumo huo kila kitu kipo wazi na hakuna anaeweza kufichwa taarifa inazohusu fedha.
Jaffo alichukua nafasi ya mweka hazina mwezi Juni mwaka huu baada ya aliyekuwepo, Dk. Titus Kamani, kuchaguliwa katika baraza la Mawaziri.