Na Halima Jumbe
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya magharibi Unguja,imesema haitasita kumchukulia hatua mwananchi yeyote atakaebainika kuvunja sheria kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Ayoub Mohammed, alieleza hayo katika ziara maalum iliyofanywa na wajumbe wa kamati hiyo katika shehia za Kombeni, Nyamanzi, Chukwani na Kiembesamaki kwa ajili ya kuangalia maeneo yanayolalamikiwa na wananchi.
Akizungumza na wawanchi hao kwa nyakati tofauti,alisema serikali imeweka mipango madhabuti kwa kila sekta ili kuhakikisha wananchi wanazitumia furasa zilizopo kwa mujibu wa sheria na kudumisha amani na utulivu.
“Sheria zilizopo zinafaa kutekelezwa na kila mwananchi, hazibagui mkubwa wala mdogo au mwenye cheo na asiye na cheo kila mmoja anapaswa kuziheshimu na uongozi wa wilaya utahakikisha unalisimamia jambo hilo,”alisema.
Wakizungumza na wananchi wa shehia za Kombeni na Dimani, wajumbe hao walipokea malalamiko ya kuwepo uharibifu wa mazingira katika eneo la kihistoria la hifadhi ya mikoko Dimani.
Ofisa kutoka idara ya misitu na mali zisizorejesheka, Mwinyi Juma Muharram, alisema taasisi yake imeanza kuyafanyia kazi malalamiko hayo kwa lengo la kuendeleza historia hiyo isitoweke.
Malalmiko mengine ni kuhusiana na ujenzi wa uzio wa ukuta kwenye shamba la Mohammed Hashim na kusababisha kuziba njia za asili zinazotumiwa na wananchi.
Nae Mwenyekiti wa kamati hiyo, aliwaahidi wananchi hao kufanya mazungumzo ya pamoja kati ya mlalamikiwa na walalamikaji na kumtaka sheha wa shehia hiyo kusimamia na kuhakikisha mivutano ya aina hiyo haiendelei tena.
Aidha kamati hiyo pia ilitembelea diko la Dimani linalolalamikiwa kutumika kama bandari bubu ya kusafirishia bidhaa za magendo zikiwemo dawa ya kulevya na bangi.
Wakitoa malalamiko yao wavuvi wa eneo hilo walidai bidhaa hizo hupitishwa katika bandari hiyo kwa kutumia gari.
Wakiwa katika eneo hilo wajumbe walifanikiwa kumkamata kijana Salmini Khamis (20) mkaazi wa Nyamanzi, akiwa katika harakati za kutaka kusafirisha vipolo 6 vya sukari na sabauni kipolo 1 kwa njia ya mgendo na kumfikisha katika kituo cha polisi Mazizini.
Hata hivyo, kamati hiyo iliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa vikosi vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa watakapowabaini watu wanaojishughulisha na vitendo viovu.
Kamati hiyo pia ilitembelea soko la samaki la Mazizini na kumuagiza Mwenyekiti wa wavuvi na madalali,Faki Haji Makame, kuorodhesha majina ya wavuvi ili wasajiliwe.
Maeneo mengine waliyotembelea ni eneo la machinjio ya ngo’mbe Kisakasaka lenye ukumbwa wa ekari 100 lilovamiwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makaazi