Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein awaambia Wakuu wa Mikoa kufahamu mipaka na majukumu kati ya uongozi na utendaji

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                      10 Novemba, 2014


TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa viongozi katika nyanja za siasa na utawala kufahamu mipaka ya majukumu yao, kujenga ushirikiano na kuwa na mawasiliano mazuri ili kuimarisha utawala bora na kufanikisha utendaji wa shughuli za Serikali.
 

Dk. Shein amesema hayo leo wakati akifungua Warsha ya Siku Tatu kuhusu Mahusiano na Mwingiliano kati ya Siasa na Utendajikwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Zanzibar na baadhi ya Tanzania Bara inayofanyika katika hoteli ya Sea Cliff nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

 

Aliwaambia washiriki wa warsha hiyo kuwa viongozi na watendaji kushindwa kuelewa majukumu na mipaka yao wakati mwingine kunasababisha baadhi yao kuyumba na kuingia katika malumbano na hatimae huathiri utendaji wao wa kazi.
 

“kuelewa majukumu yako na mipaka yake na kuyatekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa Katiba na Sheria pamoja na kuwashirikisha walio chini yako ni sehemu ya uimarishaji wa utawala bora kitu ambacho Serikali zetu zimedhamiria kukijenga” Dk. Shein aliwaeleza.
 

Alisema litakuwa ni jambo la kushangaza kwa Mkuu wa Mkoa kushindwa kupata mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake wakati kuna mfumo mzima wa uongozi ambao anauongoza kuanzia mkoani hadi katika ngazi ya shehia.



Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Hawa Ghasia, Dk. Shein alitoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu na mawasiliano kati ya viongozi wa siasa na utendaji kwa kuwa ni mambo muhimu katika kufanikisha kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchini.
 

Dk. Shein aliwaeleza washiriki hao ambao baadhi yao ni kutoka Tanzania Bara kuwa ipo changamoto kubwa ya ukosefu wa usimamizi ulio makini wa shughuli za serikali katika ngazi ya mikoa na wilaya jambo ambalo linarejesha nyuma ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
 

Kwa hivyo aliwataka kukumbuka kuwa wao ni sehemu ya uongozi hivyo hawana budi kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo ili Serikali ziweze kufikia malengo yake kama yalivyoainishwa katika mipango mbalimbali ya maendeleo pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.
 

“Tekelezeni Katiba, Sera zetu, MKUZA, MKUKUTA, Mipango mingine ya Maendeleo pamoja na Ilani yetu ya Uchaguzi ili wananchi wazidi kujenga imani kwa serikali zao” Dk. Shein alisema.
 

Katika hotuba yake hiyo ambayo alielezea pia historia na jitihada za serikali kujenga utawala wa wananchi baada ya uhuru, Dk. Shein aliwahimiza wakuu hao wa mikoa na wilaya kuendelea kushauriana, kuwasiliana na kutembeleana ili kubadilishana uzoefu na kuongeza ujuzi katika kuwatumikia wananchi.
 

Kwa upande mwingine aliwataka kuhakikisha kuwa fedha zinazopelekwa katika mikoa, wilaya na halmashauri zinatumika kulingana na matumizi yaliyopangwa na pia amewataka kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya serikali.
 

Akizungumza kumkaribisha mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alieleza kuwa katika kuimarisha Utawala katika ngazi za Mikoa na Wilaya, Baraza la Wawakilishi hivi karibuni lilipitisha Sheria mpya ya Tawala za Mikoa.
 

Kwa hivyo alisema, kufanyika kwa Warsha hiyo kumekuja wakati unaofaa kwa kuwa maudhui yake yanakwenda sambamba na jitihada hizo za Serikali kuimarisha Serikali za Mitaa.
 

Mapema akitoa maelezo kuhusu warsha hiyo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja ambayo ndio iliyoandaa warsha hiyo, alieleza kuwa lengo la warsha hiyo ni kutoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya kuongeza maarifa katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi katika utendaji.
 

Alifafanua kuwa warsha hiyo imezingatia umuhimu wa maingiliano kati siasa na utendaji katika kuleta maendeleo ya nchi na kubainisha kuwa ni muhimu maelewano hayo yakawa mazuri na yenye ushirikiano ambapo katika hali hiyo huwa ni chachu ya maendeleo na kinyume chake kuwepo kwa migongano kunadhoofisha jitihada za kuleta maendeleo ya nchi.
 

Wakuu wa mikoa kutoka Tanzania Bara wanaohudhuria warsha hiyo ni pamoja na walioteuliwa hivi karibuni ambao ni Dk. Ibrahim Msengi (Katavi), Halima Dendegu (Mtwara), Amina Masenza (Iringa) na John Mongela (Kagera). Wa zamani ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambugu na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila ambaye kabla ya mabadiliko alikuwa mkoa wa Lindi.     


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 



                                               

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles