Na Mwantanga Ame, Dar es Salaam
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar,Balozi Seif Ali Iddi, ametaja sababu za msingi zilizoifanya serikali kufanya marekebisho ya baadhi ya wizara na watendaji.Akizungumza na watendaji wa taasisi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizopo Dar es Salaam, alisema dhamira ya serikali ni kuona kunakuwa na uwiano katika baadhi ya wizara kiutendaji na kuongeza ufanisi.
Kutokanana hali hiyo,aliwataka watumishi kuyapokea mabadiliko hayo kama ni sehemu ya kuleta mafanikio.
Alisema natambua kuna changamoto ndani ya taasisi hizo na serikali itajitahidi kuona inayafanyia kazi ili kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko ya haraka na yenye nguvu na kuifanya Zanzibar kuinuka kiuchumi.
Alisema ofisi hiyo iliyopewa mamlaka ya kuratibu uwajibikaji wa Taasisi zote za SMZ zilizopo mjini Dar es Salaam hivi sasa itakuwa chini ya ofisi Makamu wa Pili wa Rais jambo ambalo litazifanya shughuli za idara hizo kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Alisema serikali iliamua kuanzisha ofisi hiyo mwaka 1986 ili iwe kiunganishi cha upatikanaji wa huduma za kiuchumi kwa urahisi.
Akizungumzia kitengo cha habari kilichojumuisha Shirika la Magazeti ya Serikali linalochapisha magazeti ya ‘Zanzibar Leo’, ‘Zanzibar Leo Jumapili’ na ‘Zaspoti’, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Idara ya Habari Maelezo, Balozi Seif aliwapongeza wanahabari hao kwa umahiri wao wa kufanya kazi licha ya kuzungukwa na mazingira magumu.
Aliuagiza uongozi wa taasisi hizo kufanya utaratibu wa kuandika mapendekezo ya vifaa muhimu zaidi vya mwanzo na kuyawasilisha serikalini.
Aliutaka uongozi wa sekta ya habari kufanya utafiti utakaofahamu tatizo linalosababisha matangazo ya ZBC kutopatikana katika maeneo ya Tanzania Bara.
Mapema Mkurugenzi wa shughuli za serikali, Shumbana Taufiq, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yake.
Nao baadhi ya watendaji wa taasisi hizo wakiwemo viongozi wao wa wizara na idara wamezitaja baadhi ya changamoto zinazokwaza utekelezaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kazi, usafiri na kuomba kuongezewa posho ili kukidhi mahitaji.
Awali Balozi Seif alitembela ofisi ya idara ya uratibu, kitengo cha utawala na rasilmali watu, uratibu wa misaada na mipango pamoja na ile ya habari.