Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Haki, Uhuru wa habari uingizwe kwenye katiba

$
0
0
Shifaa Said na Husna Mohammed
BARAZA la Habari Tanzania (MCT) na wadau wa habari wamesema kuna haja ya kuingizwa kwa kina masuala yanayohusu haki na uhuru wa habari katika rasimu ya katiba ili maoni na marekebisho hayo yawemo ndani ya katiba mpya.

Akizungumza katika mkutano wa kwanza wa baraza la katiba la tasnia ya habari lililofanyika Zanzibar, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mukajanga, alisema baraza ni muhimu kuhakikiksha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kupata habari inawekwa bayana na kwa lugha nyepesi zaidi ili wananchi waweze kufahamu na kuzitumia vyema haki hizo.

Kajubi alisema kupitia Baraza la katiba la tasnia ya habari kutakuwa na mikutano sita ambayo itafanyika katika kanda zote za Tanzania na hivyo kuna haja na umuhimu wa wajumbe wa baraza hilo kujadili kwa kina masuala muhimu ya habari na pia masuala mengine ambayo kama wananchi wanaona kuna haja ya kufanyiwa marekebisho.

“Kupitia Baraza la Katiba la Tasnia ya Habari mikutano sita iliyopangwa kufanyika katika mchakato huu, wajumbe watapata fursa ya kujadili kwa kina ibara ya 29 na 30 ambazo zinahusu uhuru wa maoni, uhuru wa habari na uhuru wa vyombo vya habari na kuviboresha ili vikidhi haja za wadau wa habari,” alifafanua.

Alisema kama baraza la tasnia ya habari hawanabudi kutoa michango yao ya kina ili yaweze kuwasilishwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo katiba iweze kuwa kamilifu kwa upande wa tasnia ya habari.

Alisema baraza la katiba la tasnia ya habari limeundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 (3) cha sheria ya mabadiliko ya katiba ambacho Tume kwa kuzingatia jiografia huunda mabaraza ya katiba nchini.

“Hili ni baraza halali la katiba na ndilo baraza pekee la kitaasisi lenye wajumbe wengi ambapo baraza hili la tasnia ya habari lina wajumbe 130kutoka sehemu zote za Tanzania,” alifafanua.

Nae Meneja wa Udhibiti na Viwango wa MCT, Pili Mtambalike, alisema ingawa ibara ya 30 na 31 imeeleza kwa kina masuala ya uhuru wa habari lakini hata hivyo kuna masuala kadhaa ambayo hayakuingizwa.

“Uhuru wa uhariri pia ni eneo ambalo halikuzingatiwa katika rasimu ya katiba hivyo kuna umuhimu wa uhuru wa uhariri kuelezwa bayana katika katiba mpya ili haki na uhuru wa habari uweze kuwepo kwa ufanisi,” alisema.

Alisema suala la haki ya kupata habari na suala la vyombo vya habari halinabudi kufafanuliwa na kupewa vifungu vya pekee kwani ilivyo hivi sasa vifungu hivi vimechanganyika na kamwe haviko bayana.

Aidha alisema uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, haki ya kufanya mawasiliano bila ya kuingiliwa ni mambo ambayo yanapaswa kuingizwa katika katiba mpya.

Nao washiriki wa mkutano huo, walisema rasimu ya katiba imewabana sana wanahabari na vyombo vyao kwa ujumla kwa kuwa imeweka mipaka katika majukumu ya kazi zao kwa ujumla.

Aidha walisema sambamba na kupewa uhuru vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla lakini katiba hiyo pia itoe haki ya kupata, kutafuta na kutoa habari kwa vyombo vya habari.

Mwandishi wa kujitegemea Enzi Talib alisema ni muhimu kwa katiba mpya kuwa na vipengele ambavyo vitaeleza bayana haja ya kuwepo chombo maalum kilicho uhuru kama vile Baraza la habari ili kuwa msimamzi mkuu wa masuala ya wana habari na vyombo vya habari.

Aidha alielezea haja ya katiba kueleza masuala yanayohusu bima na hifadhi ya wanahabari ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

“Sura ya nane ibara ya 104 ieleze bayana iwapo itatokea migogoro itatatuliwa vipi na pia suala la uwiano kiutendaji katika masuala ya habari baina ya pande mbili za muungano lielezwe bayana,” alisema.

Jasadi Bugala kutoka kituo cha huduma ya sheria Zanzibar alisema rasimu ya katiba mpya bado ina vipengele kadhaa ambavyo vimetoa uhuru kwa mkono mmoja na kupokonywa uhuru huo kwa mkono mwengine.

Akitoa mfano alisema ibara ya 30 ambayo inazungumzia masuala ya uhuru wa habari lakini bado kinawabana waandishi katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mwandishi wa kujitegemea Jabir Idriss alisema ibara ya 30 imeelezea uhuru wa habari lakini lugha iliyotumika imekuwa na kigugumizi katika suala la haki ya waandishi na vyombo vya habari.

Hasina Hamad kutoka chama cha waandishi wa habari wanawake Zanzibar alisema haki na uhuru wa habari katika ibara ya 29 na 30 ya rasimu ya katiba havina budi kuwekwa bayana na waandishi wa habari wenyewe wawe wasimamizi wakuu katika kuhakikisha vipengele hivyo vinakidhi haja ya wakati huu na baadae.

Azizi Simai kutoka Jumuiya wa Waandishi wa Habari za Mazingira Pemba,alisema suala la ulinzi wa waandishi wa habari ni muhimu hususan kwa

sasa ambapo kumezuka vitendo kadhaa vya kupoteza maisha na kutishwa kwa waandishi wa habari.

Mkutano huo wa siku moja wa baraza la tasnia ya habari uliofanyika ukumbi wa hoteli ya Mazsons ni wa kwanza kufanyika Zanzibar na umeendeshwa na Baraza la Habari Tanzania na kuwashirikisha wajumbe wa baraza la katiba wa tasnia ya habari kutoka kanda ya Zanzibar.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>