Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

SMZ yaahidi kusimama na matakwa ya wazanzibari katiba mpya

$
0
0
Kauthar Abdalla na Asya Hassan
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema itahakikisha kuwa itasimama na matakwa ya Wazanzibari kwa kuwatetea na kuwasimamia kwa yale yote watakayokubaliana katika mabaraza ya katiba katika kuleta maslahi ya Zanzibar.

Hii ni kutokana na kwamba katiba inayotakiwa na wazanzibari itabadilisha sana taifa kupitia kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hayo yameelezwa na Waziri wa katiba na sheria Abubakar Khamis Bakary wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 katika ukumbi wa Baraza la wawakilishi Chukwani.

Alisema katiba itakayopatikana itaweza kuhimili misukosuko ya kisiasa na kibinadamu na kuweza kuishi kwa miaka mingi ijayo bila ya mtikisiko wa vishindo vyovyote.

Aidha alisema kazi ya kuandaa mkakati wa mabadiliko katika sekta ya sheria imefika hatua ya kutayarishwa rasimu ya mwanzo ambayo inatarajiwa kupelekwa kwa wadau.

Waziri alisema Ofisi ya Mwendesha Mashitaka imeandaa mikakati ya uimarishaji wa usimamizi wa kesi za madai za Serikali kwa kukutana na watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma kujadili suala hilo.

Alifahamisha kuwa Ofisi hiyo imekamilisha kazi za upembuzi wa sheria ili kubaini sheria zinazotumika na zisizotumika na sasa imo katika maandalizi ya mswada wa sheria ya kufuta sheria zisizotumika.

Alisema katika hatua nyengine Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), imeanza kazi ya kufanya utafiti wa sheria zinazohusu makosa ya jinai.

Hata hivyo alisema licha ya utafiti huo lakini Ofisi ya DPP imeanza kuupitia muongozo wa mashitaka ili kuweza kuufanyia marekebisho uendane na mahitaji yaliyopo.

Nae Mjumbe wa Kamati ya katiba na sheria na utawala ya Baraza la wawakilishi, Wanu Hafidh Ameir, akiwasilisha maoni ya Kamati kuhusu bajeti hiyo alisema kwenye miradi ya maendeleo Wizara ya katiba na sheria bado inasuasua na inakwenda taratibu jambo ambalo limesababishwa na kusita kwa baadhi ya miradi yake.

Alielezea kuwa kamati imeona ipo haja kwa Wizara ya fedha kuwa makini katika uwekaji wa fedha za bajeti ili kuepuka utata kwa wajumbe hali ambayo inaweza kusababisha mzozo ndani ya Baraza hasa ikizingatiwa kuwa kuna changamoto nyingi zilizoelezwa.

Alisema kuwa tume ya kurekebisha sheria ni miongoni mwa Taasisi nyeti zilizopo hapa nchini kutokana na kwamba chombo hiki kina jukumu la kuhakikisha kuwa kinatafsiri sheria hizo katika lugha nyepesi na kuzifanya zieleweke kwa wananchi hivyo inahitaji utulivu na wataalamu wa kada tofauti zinazohusu sheria husika.

Pia alisema Ofisi ya Wakala wa usajili wa Makampuni inahitaji kuimarishwa kwa kuhakikisha inakuwa na watendaji wenye uwezo na utaalamu mkubwa kwani kamati imepata wasiwasi wa kukimbia kwa wataalamu wa Ofisi ya wakala wa usajili wa makampuni hasa katika fani za mawasiliano na Kompyuta.

Mjume huyo pia alisema kuwa kamati inaishauri Serikali kudhibiti upotevu na wizi wa kazi za wasanii kwa kuiwezesha Ofisi hii kufanya marekebisho ya sheria yake ambayo ingeweka sharti la kutorejesha leseni kwa vituo vya utangazaji ambavyo havilipi mirahaba.

Sambamba na hayo aliiomba Serikali kusaidia Ofisi ya Mrajisi wa vizazi na vifo kwa kuitafutia wafadhili kusaidia utoaji wa taaluma kwa wananchi hasa katika kukabiliana na changamoto ya kughushi vyeti vya kuzaliwa.

Akichangia bajeti hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema suala la ulaji rushwa katika Mahakama bado linalalamikiwa sana na wananchi jambo ambalo linapelekea kuwakosesha imani na chombo hicho kwani ndio sehemu inayokimbiliwa na wanyonge kupata haki zao.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk, aliwataka watendaji wanaoshugulikia Kamisheni ya Wakfu kuacha tamaa katika mali za mayatima pindi wanapogawa mirathi za marehemu.

Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa shilingi 8,188,000,000.00 kwa ajili ya matumizi ya mwaka wa fedha 2013-2014, ambapo shilingi 4,480,499,000.00 kwa matumizi ya mishahara na shilingi 3,707,501,000.00 kwa matumizi mengineyo.

Aidha imeeleza kuwa shilingi 2,154,313,000.00 kwa kazi za maendeleo ambapo shilingi 850,000,000.00 kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na shilingi 1, 304,313,000.00 kutoka kwa washirika wa maendeleo. Pia Wizara hiyo imeomba ruzuku ya shilingi 730,000,000.00 na kuchangia kwenye mfuko wa hazina shilingi 435,000,000.00.
Wawakilishi wanaendelea kujadili bajeti hiyo.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>