Na Mwantanga Ame, Dsm
JITIHADA zinazochukuliwa na Shirika ya Bima la Zanzibar (ZIC) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) zimeongeza idadi ya wateja wanaohitaji huduma katika taasisi hizo. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo alipotembelea taasisi hizo zinazotoa huduma katika jiji la Dar es Salaam.
Alisema licha ya kuvutiwa na utaratibu wao wa makusanyo lakini bado watendaji wa taasisi hizo wanapaswa kujituma zaidi kutafuta wateja wapya ili kuhimili ushindani uliopo.
Alisema mbinu ya kumchunga mteja wakati wote zitafanikiwa endapo juhudi za ziada za utoaji huduma kwa mwendo wa kasi zitachukuliwa.
Aliziomba kuendelea kujitangaza lakini pia kufikiria kuongeza matawi mengine zaidi katika maeneo yenye mkusanyiko wa wananchi.
Alisema serikali itaangalia utaratibu wa kuzikatia bima mali zake yakiwemo majengo mapya ya ofisi za serikali zinazoendelea kujengwa katika maeneo tofauti nchini.
Akitoa taarifa ya shirika la bima Zanzibar na utekelezaji wake, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Abdulnasir Abdulrahman alisema hali ya soko inaendelea kuwa ya ushindani.
Alisema biashara hiyo inachangia zaidi ya asilimia 80 ya biashara yote hali inayopelekea uongozi wa shirika kufanya juhudi za kuandikisha biashara nyengine ambazo zina faida ikilinganishwa na ya magari.
Alisema shirika limekusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kutoka katika vianzio vyake mbali mbali sawa na asilimia 86 ya lengo lake ambalo ni kukusanya shilingi bilioni 1.2.3 mwaka 2013.
Alisema katika kukabiliana na ushindani wa kibiashara shirika licha ya kufanya kazi zake Zanzibar lakini pia limeweza kujitanua kwa kufungua ofisi katika kanda za Pwani, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Mtwara.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya matawi ya benki ya watu wa Zanzibar yaliyopo Kariakoo na Lumumba jijini Dar es Salaam, Meneja wa tawi la Kariakoo, Badru Idd alisema PBZ ilipanga kuwafuata wateja wake waliopo na wanaokwenda Tanzania Bara kikazi, kibiashara, kimasomo na wanaopita ambao wanahitaji huduma za kibenki.
Alisema pamoja na ushindani uliopo matawi hayo yameweza kufungua hesabu za wateja mbali mbali na kufikia 8,360 kutoka 3,209 ikiwa ni ongezeko la asilimia 160.
Alisema amana za wateja zimefikia shilingi bilioni 24.58 mwezi Agosti mwaka huu wakati Disemba 31 mwaka 2011 zilikuwa shilingi bilioni 3.99 ikiwa ni ongezeko la asilimia 516.
Baadae Balozi Seif alikutana na uongozi wa shirika la meli na uwakala Zanzibar tawi la Dar es Salaam na kuwaasa kwamba wana kazi kubwa ya kulihudumia shirika hilo katika mazingira ya uwajibikaji.
Balozi Seif alisema shirika hilo linaweza kupoteza imani ya wateja kwa kufikia hatua ya kukata tamaa endapo uendeshaji wa taasisi hiyo hautakuwa wa kiwango.
Mapema mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifanya mazungumzo na uongozi wa shirika la biashara la Taifa (ZSTC) ambapo aliushauri kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kwa kuwapatia bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara kwa bei nafuu.