Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Transparency International limesema hali ya ufisadi inatisha nchini Tanzania ambapo matokeo ya utafiti yanaonesha huduma muhimu za kijamii zimeendelea kupatikana kwa rushwa.
Nchi nyengine iliyotajwa kushamiri ufisadi katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara ni Uganda.
"Kwenye eneo la Afrika ya Mashariki tuna takwimu ambazo zinatisha sana,kama vile Uganda au Tanzania, ambako takribani asilimia 70 ya watu wanaamini kuwa ufisadi umeshamiri. Ni jambo la kutisha zaidi kuona kwamba huduma kama vile elimu ni miongoni mwa maeneo matano yaliyoathiriwa sana na ufisadi, na hilo linayaathiri moja kwa moja maisha ya watu, maana fikiria kwamba unalazimika kutoa rushwa kutibiwa hospitalini," amesema Lucas Olo Fernandes, Afisa wa Transparency International kwa kanda ya Afrika.
Shirika hilo limesema mtu mmoja katika kila wawili duniani anaamini ufisadi umeongezeka ndani ya kipindi cha miaka miwili, ingawa watu wengi wanaamini wanaweza kubadilisha hali ya mambo.
Kupitia kile kinachoitwa "kipimo cha ufisadi ulimwenguni" cha mwaka 2013, ambacho kimechukua maoni kutoka jumla ya watu 114,000 kutoka nchi 107, shirika la Transparency International limesema ufisadi umesambaa duniani kote.
Limesema asilimia 27 ya walioulizwa, walisema wamewahi kutoa rushwa kwa ajili ya kupata huduma za kijamii ndani ya miezi 12 iliyopita, hali inayomaanisha kwamba hakuna maendeleo yoyote inapolinganishwa na muda kama huu mwaka jana, pale ripoti ya mwisho ilipotolewa.
Linalozidi kuvunja moyo, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo wa Transparency International, ni kwamba taasisi ambazo zimepewa jukumu la kupambana na ufisadi na uhalifu mwengine zenyewe haziaminiwi na wananchi.
Kwa mfano, watu katika mataifa 36 wanawaona polisi kuwa mafisadi wakubwa kabisa, kwani katika nchi hizo kiasi cha asilimia 53 ya watu walishawahi kuombwa rushwa na polisi.
Hali inafanana na hiyo kwenye taasisi za mahakama, ambapo asilimia 30 ya watu kutoka nchi 20 walishawahi kutoa rushwa mahakamani na hivyo wanaamini kuwa mfumo wa sheria umejaa ufisadi.
Hata hivyo, la kutia moyo ni kwamba, watu 9 katika kila 10 walioulizwa walisema wangelichukua hatua dhidi ya ufisadi na robo ya wale walioombwa rushwa walikataa kutoa.
Matokeo hayo yanaelezea haja ya serikali, asasi za kiraia na sekta za biashara kufanya mengi zaidi katika kuwashirikisha watu kwenye mapambano dhidi ya ufisadi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Transparency International, Huguette Labelle, serikali zinapaswa kukibeba kilio hiki cha raia dhidi ya ufisadi kwa umakini mkubwa na kuchukua hatua madhubuti kuleta uwazi na uwajibikaji.
Alisema kimsingi, serikali zimeonekana kutokufanya ya kutosha kupambana na ufisadi ndani na nje yake.