Na Asya Hassan
JESHI la Polisi Zanzibar linawashikilia watu watatu baada ya kupatikana na silaha aina ya piston inayosadikiwa kutumika katika matukio kadhaa ya uhalifu visiwani humo.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Ali Juma Mwanasai wa Dar-es-Salaam, Mohamed Said (Arnold) na Mohamed Said Mohamed wakazi wa Bububu Kigamboni.
Alisema watu hao walikamatwa baada ya polisi kupata taarifa za kuwepo watu wanaowatilia shaka kuwa wanajihusisha na vitendo vya kihalifu na matumizi ya nguvu.
Alisema kwamba baada ya kuhojiwa walikiri kuwa na silaha hiyo na hatimae walionyesha walipoficha, ambayo ilikuwa imefichwa katika shamba la migomba ikiwa imechimbiwa chini ya ardhi na kuwekwa kwenye kopo la rangi ndani ya mifuko ya plastiki.
Alisema kabla ya kukamatwa kwa silaha hiyo yalikuwepo matukio ya kihalifu yanayohusisha matumizi ya silaha yaliyojitokeza likiwemo tukio lililotokea Mbuyuni Mjini Unguja Aprili 4 mwaka huu saa 11:00 jioni ambapo wahalifu walifyatua risasi na baadae kukimbia.
Tukio jengine ni lile lilitokea eneo la Mlandege Mei 13 mwaka huu majira ya saa 8:30 mchana ambapo wahalifu walifyatua risasi moja lakini hawakupata kitu.
Kamishna Mussa alisema katika tukio jengine lililotokea Kiembesamaki Mei 25 mwaka huu majira ya saa 4:45 usiku wahalifu walifanikiwa kuiba milioni 1,040,000 na vocha za shilingi milioni nne.
Katika matukio mengine ya matumizi ya silaha, wahalifu walijaribu kuiba na kutishia kufyatua risasi, tukio ambalo lilitokea Kikwajuni Juni 21 mwaka huu majira ya saa 1:30.
Kamishna Mussa pia alikumbushia tukio la shambulizi la Padri Ambros Mkenda lililotokea Diesemba 26 mwaka jana saa 2:00 usiku huko Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja alipoigwa risasi kichwani na tukio la kuuliwa kwa Padri Mushi Februari 17 mwaka huu saa 1:00 asubuhi huko Betrass Unguja.
“Kutokana na kukamatwa kwa bastola hii tunaendelea kuwahoji watu hawa kwa kina zaidi ili kubaini kama matumizi ya bastola hii inahusishwa kati ya moja ya matukio haya, pia tunataka kujua washiriki wao wengine katika matukio haya, watu wanaowafadhili kwa kuwapa taarifa zinazowawezesha kufanya uhalifu na watu wanaowapa usafiri kufanikisha uhalifu huo,” alisema.
Alibainisha kwamba dalili za kuwapata wahusika wengine zipo kwani watu hao waliokamatwa weameanza kuelezea washirika wao na mipango ya kihalifu iliyotarajiwa kufanyika baadae na kuahidi kwamba jeshi la polisi liko makini na wahusika wote hao watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Akizungumzia mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani , aliwataka wananchi kuendelea kuwa makini na kushirikiana ipasavyo na polisi katika harakati zote za kupambana na uhalifu na wahalifu.
Alisema uzoefu unaonyesha kwamba katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani baadhi ya makosa ya jinai huongezeka ikiwemo ajali za barabarani, wizi wa kuvunja nyumba usiku, kuibiwa vyombo vya maringi mawili zikiwemo vespa , pikipiki na wizi wa mazao.
Kamishna Mussa alisema kubwa zaidi linalotishia ni kuvamiwa na kuibiwa fedha katika vituo vya petroli nyakati za jioni wakati watu wengi wakiwa nyumbani kwa kupata futari.