Na Ali Issa, Maelezo
WAZIRI wa Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar, Nassour Ahmed Mazrui, amesema lengo la wafanyabiashara wa China kuja Zanzibar ni kutoa fursa pana zaidi ya uwekezaji, kuinua uchumi na kutoa ajira kwa vijana.Hayo aliyasema jana katika hoteli ya Grand Palace Malindi wakati wa ufunguzi wa mkutano kati ya wafanyabiashara wa Zanzibar na wawekezaji kutoka China ambao wamekuja Zanzibar kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi.
Alisema azma hiyo ni muelekeo mzuri na fursa pekee kwa Zanzibar ambayo ni kisiwa kinachohitaji kukuza uchumi wake kupitia sekta ya uwekezaji wa biashara.
“Ni faraja kubwa kwa Zanzibar kupokea wageni wa aina hii kwani karibu duniani kote hivi sasa kuna ushindani mkubwa wa kuwavuta wawekeza ili kuinua uchumi wa nchi zao,” alisema.
Alisema wawekezaji hao wanatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa serikali kwa kuwekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu na sekta nyengine za biashara.
Alisema China na Zanzibar ni marafiki wa muda mrefu na zimekuwa zikisaidia katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya, masuala kifedha na ujenzi wa miundombinu.
Nae Balozi Mdogo wa China aliepo Zanzibar, Chen Qiman akiutambulisha ujumbe wa wafanyabiashara hao alisema wameamua kuja Zanzibar kuwekeza kutokana na vivutio vizuri vilivyopo na ni sehemu yenye utulivu.
“Wafanyabiashara hao wataangalia uwezekano wa kuwekeza katika maeneo ya uvuvi, utalii na sekta nyengine za maendeleo ambazo hazina mashaka kuzifikia,” alisema Balozi Chen Qiman.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Nassour Hassan, aliwahakikisha wafanyabiashara hao kuwa Zanzibar ina maeneo mazuri ya uwekezaji vitega uchumi ambayo yanaweza kufikiwa kwa urahisi na yamewekewa miundombinu ya kutosha.
Aliwaeleza wageni hao kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kuwekeza ikiwemo fukwe za kuvutia, maji safi na aina mbali mbali za viungo ambavyo hutumika kwenye chakula, vinywaji, kutengenezea bidhaa na baadhi yao hutumika kama tiba.
Alisema Zanzibar imepiga hatua katika masuala ya usafiri wa anga bahari kwa kuufanyia marekebisho makubwa uwanja wa ndege wa Zanzibar na kuitanua bandari ya Malindi.
Kuwasili kwa wawekezaji hao kunatokana na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoifanya nchini China hivi karibuni na kukutana na wawekezaji ambao walifurahishwa na maelezo waliyopata.