Na Mwandishi wetu
JUMUIYA ya UVCCM wilaya ya Dimani,imeunga mkono uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM uliotolewa Dodoma wa kumvua uanachama aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembe Samaki, Mansoor Yussuf Himid.Taarifa iliyotolewa na Katibu wa UVCCM wilaya hiyo,Yussuf Ramadhan imeelezea kuwa umoja huo umepata faraja na imani kubwa kuona chama chao kikichukua na kufuata mkondo wa kinidhamu kukabiliana vurugu zilizokuwa zikifanywa na Mwakilishi huyo.
Alisema uamuzi huo usiishie kwa Mansoor pekee bali wanataka kila Mwakilishi, Mbunge na kiongozi yeyote wa CCM anaekwenda kinyume na sera za chama hicho achukuliwe hatua.
Alisema bado kuna Wawakilishi wengine wanaotoa matamko ya kukikebehi na kukikejeli chama huku kauli na misimamo yao ikiwa haina tofauti na ile ya upinzani.
Alisema umefika wakati kwa CCM kuwachukulia hatua za kimaadili Wawakilishi na Wabunge ambao mchana ni wana CCM na usiku hugeuka na kuwa maadui na wasaliti.