Na Haji Nassor, Pemba
BENKI Watu wa Zanzibar (PBZ), imeanzisha huduma mpya ya kibenki kupitia simu ya mkononi (mobile bank), itakayowarahisishia wateja kujua akiba yao, kulipia maji, umeme na huduma nyengine zilizosajiliwa na benki hiyo.Akizungumza na watendaji wa wakuu wa serikali kisiwani Pemba hivi karibuni, Mkurugenzi masoko wa benki hiyo, Viwe Ali Juma, alisema PBZ imeamua kuanzisha huduma hiyo, kwa lengo la kupunguza msongamano katika matawi yake.
Alisema huduma hiyo ambayo kujiunga kwake ni rahisi, anaamini itawasaidia wateja wao, kulipia ankara zao za huduma kama vile maji na umeme na kununua vocha za simu.
Mkurugenzi huyo, aliwashauri watendaji hao kuhakikisha wanawaelimisha wafanyakazi wao juu ya kuanzishwa kwa huduma hiyo, ambayo pamoja na mambo mengine ni rahisi kuitumia.
Alieleza kuwa pia huduma hiyo itamuwezesha mteja ambae ameshasajiliwa kutumia huduma ya kibenki kwa njia ya simu ya mkononi, kuhamisha salio kutoka kwenye akaunti yake na kumpekelekea mwenzake.
Katika hatua nyengine, alisema tayari PBZ imeanza kutoa mikopo ya nyumba kwa wateja wake baada ya kukamilisha taratibu husika.
‘’Wafanyakazi sasa njooni benki yenu ya PBZ, maana mikopo ya nyumba ipo, ukikamilisha masharti tu, unatoka na nyumba yako na unakatwa taratibu,”alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa Idara ya benki ya kiislamu kutoka benki ya watu wa Zanzibar tawi la Chake Chake, aliwataka wateja kuhamia kwenye idara hiyo kuchukua mikopo ambayo haina riba.
Alisema mikopo inayotolewa na benki ya kiislamu, ndio pekee ambayo imefanyiwa utafiti na kuonekana inaweza kukuza pato na kuinua uchumi wa hata mtu mmoja mmoja.
Baadhi ya watendaji wa Serikali wakichangia katika mkutano wameishauri PBZ kuimarisha huduma zake, ikiwa ni pamoja na kusambaza mashine za ATM ili kuondoa msongamano hasa siku za mishahara.