Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein : Tunalipa uzito suala la ulinzi na usalama wa wageni

$
0
0
Na Said Ameir, The Hague, Uholanzi
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa Serikali yake inalipa uzito mkubwa suala la ulinzi na usalama nchini na hatua za kipekee zinachukuliwa katika maeneo ya kitalii kwa kuwa sekta hiyo ni sekta mama kwa uchumi wa Zanzibar.
 
Dk. Shein ametoa kauli hiyo jana wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Biashara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Uholanzi Bibi Lilianne Ploumen ambapo walizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uholanzi.
 
“tunalipa uzito mkubwa suala la usalama nchini kwetu na tumeandaa mpango maalum wa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya kitalii” alibainisha.
 
Alimueleza Bibi Lilianne kuwa sekta ya utalii ni sekta mama ya uchumi wa Zanzibar ambayo inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni hivyo Serikali inachukua kila hatua kuimarisha sekta hiyo ikiwemo kuwahakikishia usalama watalii na wageni wanaotembelea Zanzibar kila siku.
 
Alisema kuwa taarifa za tukio la kuteketea kwa moto kwa hoteli ya Paradise iliyoko katika fukwe ya Marumbi, Wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja hivi karibuni limemshitua na kumsikitisha na kueleza kuwa vyombo husika vya Serikali vimechukua hatua zinazostahiki kushughulikia tukio hilo.
 
“taarifa tulizonazo hadi sasa tukio hilo ni ajali ya kawaida” alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa anashukuru kuwa hapakuwa na madhara makubwa kwa watalii na watumishi wa hoteli isipokuwa majeruhi kidogo kwa watu wawili tu.
 
Dk. Shein amesema ziara yake nchini Uholanzi imelenga kuangalia maeneo mapya ya uhusiano na ushirikiano ikiwa ni miongoni mwa jitihada za nchi mbili hizo kuimarisha uhusiano huo uliodumu kwa miongo mingi.
 
“tumekuwa na uhusiano mzuri kwa miaka mingi na tumekuwa tukishirikiana katika maeneo kama ya elimu, afya, miundombinu na kadhalika hivyo tumeona sasa ni wakati muafaka kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya nchi na watu wetu”alieleza Dk Shein.
Aliyataja baadhi ya maeneo mapya ya ushirikiano kuwa ni pamoja na sekta ya nishati, uvuvi wa bahari kuu,miundombinu na kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii.
 
“tungependa kuona uwekezaji zaidi katika sekta ya utalii na kuvutia watalii wengi kutembelea Zanzibar na mbuga za wanyama”alisema.
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali na wananchi wa Uholanzi kwa misaada yake mbalimbali kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
 
“wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakifaidika na misaada mingi ya kimaendeleo ambayo imekuwa chachu katika kusukuma gurudumu la maendeleo yetu”alieleza na kutaja sekta ya elimu na uimarishaji wa sekta ya afya kuwa miongoni mwa misaada hiyo.
 
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Balozi Diodorus Kamala na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia.
 
 
 
Wakati huo huo Serikali ya Uholanzi imesema iko tayari kushirikiana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendeleza sekta ya nishati kwa kuipatia utaaalamu na uzoefu katika kusimamia na kuendeleza sekta hiyo.
 
Hayo yameelezwa na Waziri wa Biashara ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bibi    Lilianne Ploumen wakati alipokutana Rais wa Zanzibar jana.
 
“tuna utaalamu mkubwa na uzoefu wa miaka mingi katika kubuni, kusimamia, na kuendesha sekta ya nishati...tuko tayari kushirikiana na nanyi kutumia utaalaamu na uzoefu wetu kuimarisha sekta hiyo”alisema Waziri huyo.
 
Bibi Ploumen alisema ziara ya Rais wa Zanzibar na ile aliyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete zimefanyika wakati muafaka ambapo jitihada za kuimarisha uhusiano kati ya Uholanzi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaelekezwa katika kuunganisha nguvu kwenye biashara na uwekezaji.
 
Waziri huyo alisema nchi yake inashukuru kupewa fursa ya kuchangia maendeleo ya sekta ya afya na kwamba mchango huo unasaidia katika kuifanya Zanzibar iweze kufikia malengo ya milennia katika suala la afya.
 
“Nimefurahi kuwa nchi yetu imepewa fursa ya kushiriki katika kuimarisha sekta ya afya huko Zanzibar na mchango wetu utasaidia Zanzibar kufikia malengo ya milenia kwa kupunguza vifo vya watoto na vile vya kina mama vinavyotokana na uzazi”alieleza Bibi Ploumen.
 
Katika mazungumzo hayo Bibi Ploumen aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi kwa hatua za haraka ilizochukua kuhusiana na tukio la kuungua moto hoteli ya Paradise huko Marumbi.
 
“Tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi kwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia ajali hiyo na tunashukuru kuwa hakukuwa na madhara kwa watu”alisema na kueleza matumaini yake kuwa tukio huo halitaathiri biashara katika sekta hiyo.
 
Rais wa Zanzibar anaendelea na ziara yake ya siku tano nchini Uholanzi ambapo leo Alhamisi atakutana na Waziri Mkuu wa Uholanzi Bwana Mark Rutte, atatembelea Kampuni ya vifaa vya uchunguzi wa maradhi ya Sakura ambako atabadilishana mawazo juu ya masuala ya afya kati ya Zanzibar na Uholanzi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles