Kauthar Abdalla na Mwashamba Juma
MTUHUMIWA wa mauaji ya shemegie aliekuwa akitafutwa kwa muda mrefu hatimae amekamatwa akiwa amejificha katika msitu wa Paje, wilaya ya Kusini Unguja.
Mtuhumiwa huyo Silvesta Robert Masharo (42) mkaazi wa Paje alikutwa na wananchi akiwa amejificha katika msitu huo na watu waliokuwa katika kazi zao za kawaida katika msitu huo.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Augustino Ollomi alisema mtuhumiwa alikamatwa Agosti 22.
Wakati wakiwa huko alikuwa akila matunda ya porini kwa sababu hakuwa na chakula wala fedha.
Kamanda Ollomi alisema jalada la mtuhumiwa limeshatumwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya ushahidi kukamilika.
Katika tukio jengine, Kamanda alisema mzee mwenye umri wa miaka 70 alietajwa kwa jina la Asya Milango Mayaya (70), mkaazi wa Kiboje Mkwajuni alikutwa akiwa amekufa nyumbani kwake majira ya saa 1:30 asubuhi.
Hata hivyo, Kamanda Ollomi hakutaja sababu za kifo chake ingawa uchunguzi wa waandishi wa habari hizi umethibitisha kwamba kifo chake huenda kimesababishwa na majeraha baada ya kudaiwa kubakwa na watu wasiojulikana.
Alisema mzee huyo alikuwa akiishi peke yake hadi kifo kilipomkuta na kwamba hakuwahi kuumwa.
Aidha alisema mazingira ya nyumbani kwake hayakuwa ya kawaida, hali inayoonesha kwamba kabla ya kifo chake kulikuwa na mapambano kati yake na watuhumiwa.
Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa taratibu za mazishi na uchunguzi unaendelea.
Katika tukio jengine, hoteli ya kitalii ya Paradise iliyopo Marumbi imeungua na kusababisha hasara ya vitu kadhaa.
Alisema hoteli hiyo inamilikiwa na raia wa Uholanzi anaeitwa Belty Schoomvemde ambapo nyumba tatu zilizokuwa jirani pia zimeungua.
Alisema moto huo uliunguza majengo 16 yenye vyumba 56 vya wageni, bweni moja la vyumba saba vya wafanyakazi, gari, pikipiki na baskeli nne.
Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.