Na Hussein Makame, Maelezo
MWANASIASA mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru, amewataka Watanzania wasikubali kuyumbishwa kama nchi kuhusu umoja wa kitaifa, udugu,mshikamano,amani na utulivu wakati wa mchakato wa kutoa maoni ya kuunda katiba mpya.Kingunge alitoa angalizo hilo kwenye mkutano wa kufunga rasmi mabaraza ya katiba yaliyo chini ya Chama cha Watabibu wa Tiba Asili (ATME) uliofanyika mjini Bagamoyo.
Mwanasiasa huyo alitoa angalizo hilo baada ya kueleza kuwa kuna baadhi ya watu wakiwemo wanasisasa kutoa maoni ya kuunda katiba mpya yanayolenga kuvuruga umoja wa kitaifa, udugu, mshikamano, amani na utulivu uliopo.
“Kwa sasa Tanzania umoja wa kitaifa tulionao umetufikisha pazuri, kwenye udugu na mshikamano, lakini kwenye utulivu na amani hali si nzuri sana baada ya kujitokeza watu wanaotaka kuuchafua,” alisema.
“Kwa hivyo tusikubali kuyumbishwa kama nchi,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.
Aliwambia Watanzania watoe mawazo ya kujenga na sio mawazo ya kuwagawa Watanzania na kuwafanya waishi katika maisha yatakayoliangamiza taifa miaka ijayo.
Alisema kuna mwanasiasa mmoja visiwani Zanzibar aliwahi kusema kuwa Rais wa kwanza wa visiwa hivyo, Mzee Abeid Amani Karume alitishiwa kuukubali muungano ndio mana akafanya hivyo, jambo ambalo alisema sio sahihi.
Akizungumzia tiba asili, Kingunge alikitaka ATME kwanza wajenge uhalali wa shughuli zinazofanywa na wanachama wake kwa kuanza kupiga vita upotoshaji wa wale ambao si watibabu wa tiba asili.
Aliongeza kuwa tiba asili zipo na hazihitaji kupotoshwa na watabibu wa tiba hizo wanaoendesha kwa kuchanganya na ramli wanafanya ujanja na upotoshaji.
Aliwashauri ATME na wanachama wake kujikita katika kufanya utafiti wa tiba mbalimbali na kutafuta ukweli juu ya mambo muhimu kwani kufanya hivyo watapata maarifa mengi ya kuwasaidia kutoa tiba kwa uhakika.
Akisoma risala ya ATME, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Othman Shem alisema katika mabaraza ya katiba yaliyoandaliwa chini ya chama hicho, wameshirikisha mikoa 25 na wilaya 133.
Alitaja baadhi ya mambo yaliyopendekezwa kwenye mabaraza hayo kuwa ni katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaje tiba asili kuwa ni huduma ya siha, haki za binadam nau liwe suala la muungano na rasilimali za taifa ziwe za Muungano.
Mabaraza hayo ya katiba chini ya ATME yalianza mikutano yake mwishoni mwa mwezi uliopita na baada ya kufunga mabaraza hayo, chama hicho kinawasilisha maoni yao leo Agosti 30 kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.