Na Mwandishi wetu
MWANAJESHI mmoja wa Tanzania mwenye cheo cha Meja, ameuawa mjini Goma Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya kuangukiwa na bomu akiwa pamoja na wenzake.
Taarifa kutoka Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) makao makuu Upanga jijini Dar es Salaam, imesema mwanajeshi huyo Meja Khatibu Mshindo alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitali pamoja na wenzake.
Tukio hilo limetokea Agosti 28 wakati wanajeshi wa Tanzania wakiwa katika eneo lao la ulinzi.
Taarifa hiyo imesema majeruhi wengine ambao hawakutajwa idadi yao wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.
Taratibu za kuusafirisha mwili wa afisa huyo zinafanywa.
Wanajeshi wa JWTZ wanashiriki katika operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani huko Goma, DRC.
Hata hivyo jana, Umoja wa Mataifa ulisema mwanajeshi wake mmoja wa kulinda amani ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia mapigano makali kati yao na waasi Mashariki mwa DRC.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Farhan Haq, hata hivyo hakutaja uraia wa mwanajeshi alieuuawa na waliojeruhiwa.
Alisema wanajeshi hao walitumia helikopta kuwasukuma nyuma wapiganaji wa M23 karibu na mji wa Goma, ambao ndio mji mkubwa zaidi katika eneo hilo la Mashariki.