Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Kamishna wa Polisi Zanzibar Akanusha Kusimamishwa Kazi. Akiri Upanga wa SARPCCO Kupotea

$
0
0
Na Mwantanga Ame
KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, amekanusha uvumi ulioenea kwamba amesimamishwa kazi kutokana na kinachodaiwa kupotea upanga maalum wa Jumuiya Majeshi ya Polisi kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SARPCCO).

Uvumi wa Kamishna huyo kusimamishwa kazi umeenea katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Upanga huo ni alama maalum ya kipolisi inayokabidhiwa nchi mwenyeji wa mkutano wa SARPCCO.

Mwaka jana mkutano huo ulifanyika Zanzibar katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort, ambapo Tanzania ilikuwa ndio mwenyeji.

Upotevu wa upanga huo, umedaiwa kumuhusisha Kamishna huyo, kwa vile ndie aliyedaiwa kukabidhiwa baada ya sherehe ya makabidhiano.

Upanga huo unadaiwa umesarifiwa kwa madini ya dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Kamishna Mussa, alisema taarifa hizo ni za kweli na anafahamu uvumi huo, lakini sio kweli kuwa amesimamishwa kazi.

Alisema bado yuko kazini, lakini amekiri kwamba upanga huo umepotea na haujulikani ulipowekwa.

Alisema upanga huo, ulipotea katika mazingira ya kuutatanisha baada ya kuupokea kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema.

“Unajua nidhamu zetu za kijeshi, IGP Mwema, alipokea ule upanga sasa yeye hawezi kukaa nao pale kuna walinzi wetu, ambao ni wasaidizi wake sasa hapo alipokelewa na hatujui uliishia wapi,” alisema.

“Tabu yenyewe inakuwa kubwa kutokana na kitu chenyewe hakisemi ndio maana tumelazimika kukitafuta kwa hiyo bado tunaendelea kukitafuta na huo uvumi unaosemwa wote ni uongo, mimi nipo kazini hapa tunapozungumza na wewe, na hizo taarifa mimi nazisikia zipo mitaani nimefukuzwa kazi,” alisema.

Alisema tayari wameanza kuwahoji baadhi ya watendaji wa jeshi ili kufahamu ni wapi upanga huo uliishia.

Habari za uhakika kutoka polisi, askari watano wameanza kuhojiwa juu ya suala hilo, baada ya kuwasili timu ya makachero kutoka makao makuu ya polisi mjini Dar es Salaam.

Baadhi ya askari waliohojiwa ni pamoja na Mkuu wa polisi wa wilaya ya mjini, aliefahamika kwa jina moja la SSP, Issa na SP Omar ambaye ni Mkuu wa kituo cha polisi cha Malindi na baadhi ya askari wa kikosi cha kuzuiya fujo (FFU).

Alisema jeshi hilo limeamua kutengeneza upanga mwengine kwa ajili ya kuupeleka katika mkutano wa nchi wanachama unaotarajiwa kufanyika Namibia.

Alisema yeye binafsi hajawahi kuushika upanga huo, zaidi ya kuuona kwa mbali tangu ulipokabidhiwa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>