Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Viongozi CCM Kisonge Wangolewa kwa Kukiuka Maadali, Ubadhilifu. Wenyewe Wadai ni Maamuzi Binafsi, Hawayatambui.

$
0
0
Na Salum Vuai, Maelezo

SUITAFAHAMU imeikumba maskani ‘kaka’ ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Muembekisonge, kufuatia uongozi wa Wadi ya Rahaleo kutangaza kuwang’oa viongozi wa maskani hiyo kwa madai ya kukiuka maadili na ubadhirifu.

Wakati uongozi wa Wadi hiyo ukianika bayana hatua yake ya kuwafyeka viongozi wa maskani hiyo maarufu nchini, viongozi hao wamesema hawatambui maamuzi hayo na kwamba bado wanaiongoza maskani hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika tawi la CCM Muembeshauri, Katibu wa Wadi hiyo, Abdalla Mohammed Abdalla, alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuinusuru maskani hiyo na kulinda heshima ya chama ambayo imejijengea kwa miaka mingi mbele ya jamii ya Wazanzibari.

Alisema Halmashauri ya Wadi hiyo ilifanya kikao Juni 29, mwaka huu na kuongozwa naye baada ya kupata baraka za Mwenyekiti wa Wadi ambaye kwa wakati huo alikuwa safarini nje ya kisiwa cha Unguja, ambapo wajumbe 30 walihudhuria.

Alisema tayari viongozi hao wameshakabidhiwa barua zinazowataarifu hatua ya kuvuliwa uongozi, zilizoandikwa Julai 1, 2013, na kutiwa saini na Katibu huyo.

Katibu huyo alionesha nakala ya barua iliyotumwa kwa mmoja wa viongozi hao, ambayo iliwataka kutekeleza maamuzi hayo ya chama na kushirikiana na viongozi walioteuliwa kukaimu nafasi zao kwa kuwakabidhi mali, vifaa na vitendea kazi vyote vya maskani kwa mujibu wa maelekezo ya uongozi wa tawi la CCM Muembeshauri.

“Napenda kukujuilisha rasmi kuwa, katika kikao chake cha tarehe 29/06/2013, Halmashauri Kuu ya CCM Wadi ya Rahaleo, ilizingatia na kujadili ripoti za kamati zake za (1) Siasa na (2) Usalama na Maadili na kufikia uamuzi wa kuuondosha madarakani uongozi wa maskani Kisonge ambao awali ulikuwa umesimamishwa,” iIisema sehemu ya barua hiyo.

“Halmashauri Kuu ya Wadi inapenda kukukumbusha kuwa, kukaidi maamuzi haya na maelekezo yaliyotolewa ni kosa chini ya vifungu vya katiba na kanuni za CCM na inaweza kusababisha kuchukuliwa hata zaidi,” alieleza Abdalla kupitia barua hiyo.

Viongozi waliong’olewa madarakani ni Hussein Mohammed Chwaya (Mwenyekiti), Mzee Yunus Haji (Katibu), pamoja na wajumbe Issa Suleiman Issa, Zahran Abdulrazak Mussa ‘Kwacha’ na Shaaban Ramadhan (Kocha).

Katibu huyo wa Wadi ya Rahaleo, aliwataja wanachama walioteuliwa kukaimu nafasi hizo huku maandalizi ya uchaguzi wa kujaza viti hivyo yakiendelea, kuwa ni Mbarouk Abdalla Hanga (Kaimu Mwenyekiti), Kassim Juma Tindwa (Katibu), ambapo wajumbe ni Haji Sultan Tembe, Zuhra Mgeni Mwalimu na Rukia Mohammed Othman.

Akifafanua sababu za msingi za kuenguliwa kwa viongozi hao, Mwenyekiti wa Wadi hiyo Zahran Omari, alisema kwa ujumla viongozi hao wamekuwa na tabia ya kukiuka maadili ya uongozi na utawala, na kufanya ubadhirifu wa mali za maskani hiyo.

“Kwa mfano kufanya maamuzi muhimu bila kuishirikisha Halmashauri na wanachama wengine, kushindwa kutoa taarifa za fedha za chama kwa muda mrefu, na kufanya mambo mengi kwa utashi na ushabiki tu ambayo yanakipa chama chetu taswira mbaya na ni mambo yasiyoweza kuvumilika,” alisema.

Hata hivyo, alipobanwa ili aeleze kwa uwazi ubadhirifu na utashi uliofanywa na viongozi hao, Mwenyekiti huyo alisema, “itoshe tu kukwambieni kwamba viongozi hawa wamekiuka maadili ya uongozi na utawala, humo kumebebwa kila kitu yakiwemo hayo ya ubadhirifu.”

Alifahamisha kuwa kwa kuzingatia hadhi na jina kubwa la maskani ya Kisonge nchini, na historia yake katika kukiimarisha Chama cha Mapinduzi na kuwaunganisha wanachama wake nchi nzima, alisema, haijuzu kuona mambo yanakwenda ovyo na kuyafumbia macho.

“Kumekuwa na suitafahamu kubwa, viongozi wamepewa dhamana kwa kuaminiwa lakini wanakwenda kinyume na katiba, miongozo ya chama na maadili ya uongozi. Lazima hatua za haraka zichukuliwe hasa tukizingatia tunakabiliwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema.

Gazeti hili halikutosheka na kauli za viongozi hao wa Wadi na likaamua kumtafuta Mzee Yunus Haji, Katibu aliyetangazwa kuondolewa madarakani ambaye alisema wao hawayatambui maamuzi hayo na bado ni viongozi halali wa maskani hiyo.

Alielezea kushangazwa na maamuzi hayo, akisema yamefanywa kwa utashi binafsi bila kufuata taratibu za kichama kuwakutanisha wanachama ili wajue kinachoendelea ili nao watoe mawazo yao.

Yunus alisisitiza kuwa wao bado ni viongozi wa maskani hiyo, na akatoa ushahidi wa mkutano wa wanawake walioufanya Jumatatu iliyopita tawini hapo, ambao alisema ulikwenda vizuri, huku wanachama hao wakiwataka waendelee kuiongoza maskani hiyo.

Aidha, alisema kwa mujibu wa taratibu za CCM, Halmashauri ya Wadi haina mamlaka ya kuondosha viongozi, bali wanachoweza ni kuwasimamisha tu, lakini kwa sababu za msingi na sio kama walivyofanya wao kuwang’oa bila ya kuweka wazi sababu ili zifahamike na kila mtu.

“Sisi hatujui kosa letu, wala wanachama hawajui, haya mambo yamefanywa kwa utashi na maslahi binafsi tu, halafu wanataka kufanya uchaguzi wakati chaguzi zote za chama zimemalizika, na hata Rais Dk. Shein amesema sasa hakuna uchaguzi zaidi wa taifa mwaka 2015,” alifafanua Yunus.

Alisema kabla ya hatua hiyo, uliitishwa mkutano wa wanachama wote na wakatakiwa wawe kitu kimoja na viongozi lakini uongozi wa Halmashauri ukaamua kuunda kamati mbili ya fedha na nyengine ya ujenzi, na kuweka watu wao kuziongoza.

Hata hivyo, alisema hatua ya kuunda kamati hizo ndio iliyoibua suitafahamu yote hiyo, ambapo alisema viongozi waliowekwa kuziongoza hawakuridhiwa na wanachama, kwani huko nyuma hawakupitishwa kwenye chaguzi za chama hicho.

Yunus alieleza kuwa, tayari yeye na wenzake walioenguliwa katika uongozi wa maskani hiyo wamepeleka malalamiko yao wilayani na wametakiwa kusubiri.

Katika hatua nyengine, alisema Jumamosi ya wiki hii wanapanga kuitisha mkutano mkubwa wa wanachama utakaoanza saa 4:00 asubuhi katika maskani hiyo kujadili hatua iliyochukuliwa na Halmashauri ya Wadi ya Rahaleo na uhalali wake.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>