Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

SMZ Yaipongeza SMT Kuteketeza Unga Mbovu.

$
0
0
Na Mwajuma Mmanga, Naima Hamza, MSJ

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kwa kufanikisha kazi za kuondoa unga wa ngano mbovu jumla ya makontena 30 katika bandari ya Malindi na kuupeleka Tanzania Bara kwa ajili ya kuteketezwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji alisema hayo wakati alikitoa ufafanuzi kuhusu kazi za kuangamiza unga wa ngano mbovu katika bandari ya Malindi na kusababisha usumbufu mkubwa.

Fereji alilazimika kutoa ufafanuzi huo kufuatia baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutaka kupewa maelezo kuhusu unga wa ngano ambao ulioharibika na kukaa katika bandari hiyo kwa zaidi ya miezi saba huku ukileta harufu kali.

Alisema unga huo tayari umepelekwa Tanzania Bara kwa ajili ya kuangamizwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira.

“Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia kuangamiza unga wa ngano makontena 30 ambacho ni kiwango kikubwa kutokana na udogo wa kisiwa cha Unguja hatuna sehemu ya kuangamiza unga huo,”alisema.

Waziri Fereji alisema kazi za kuchukua unga huo na kuupeleka Tanzania Bara kwa ajili ya kuteketezwa zilianza Juni 1 na kumaliza Juni 8 na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana tayari jumla ya makontena 15 yameteketezwa kwa sasa.

Mazungumzo ya kuteketeza unga huo yalifanywa katika kikao cha pamoja katika nyakati tofauti kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Therezia Huviza pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Fatma Abdulhabib Fereji.

Mapema Fereji alitoa wito kwa wafanyabiashara kuwa makini katika uingizaji wa bidhaa na kuhakikisha kwamba zinakuwa salama kwa ajili ya matumizi ya walaji.

Alisema kwa mujibu wa mazingira ya visiwa vya Zanzibar na udogo wake ni vigumu kupata eneo la kuangamiza bidhaa zilizokwisha muda wake wa matumizi.

Unga huo uliingizwa nchini na kampuni ya Bopar na kupigwa marufuku kutumika baada ya kubainika kwamba ni mbovu na haufai kwa matumizi ya binaadamu.

Hata hivyo kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kuangamiza unga wa huo ambao ni kiasi kikubwa kwa hivyo Serikali ililazimika kuingilia kati kwa ajili ya kuuteketeza na kuomba msaada kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>