Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

SMZ Kesi za Udhalilishaji Hazipati Hukumu Stahiki. Wawakilishi Wataka Utafiti wa Unyanyasaji Wanaume.

$
0
0
Na Khamis Amani

KESI nyingi za udhalilishaji wa kijinsia zinazoripotiwa Unguja na Pemba hazipati hukumu ipasavyo, kutokana na mapungufu mbali mbali hali inayosababisha kushamiri kwa vitendo hivyo.

Hivyo imeshauriwa kuanzishwa kwa mahakama maalumu (special session) kwa lengo la kuharakisha uendeshaji wa kesi za udhalilishaji.

Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed aliyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.

Kufuatia suala hilo, Wizara inaendelea kuratibu shughuli za kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika ngazi zote.

Waziri Zainab alisema ili kuona suala hilo linafanikiwa, wizara imefanya ukaguzi wa vituo vinavyotoa huduma kwa waathirika wa vitendo vya udhalilisha ikiwemo hospitali, mahakama, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na polisi Unguja na Pemba, ili kutathmini kama utoaji wa huduma unaendana na taratibu na sheria zilizopo na kushauriana jinsi ya kuimarisha huduma hizo.

Alisema kamati maalumu ya viongozi wa juu imekutana na kuweka mikakati ya kuharakisha ushughulikiaji wa kesi za udhalilishaji wanawake na watoto na kusisitizwa kuwepo kwa mahakama maalumu kwa lengo la kuharakisha kesi hizo.

Waziri Zainab alisema, katika hatua ya kufanya tathmini ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto (GBV Operational research) umebaini ukatili wa kingono ndio mkubwa zaidi ukifuatiwa na udhalilishaji wa majumbani.

Alisema vitendo vingi vya udhalilishaji wanawake haviripotiwi kutokana na aibu ukilinganisha na vya watoto matokeo ambayo yatawezesha Wizara kufanya maamuzi ya kisera, mipango na utekelezaji.

Kuhusu malalamiko yanayopokelewa wizarani kwake kuhusu masuala ya ndoa, alisema wizara imefanya tathmini ya sheria ya ndoa sura ya 91 ya mwaka 1915 na sura ya 92 ya mwaka 1936 ili kubaini mapungufu yaliyomo katika sheria hiyo.

Alisema tathmini hiyo imebaini kuwa sheria hizo zimepitwa na wakati na zina mapungufu kadhaa yakiwemo sheria hizo kujikita zaidi katika masuala ya usajili bila ya kuweka misingi muhimu ya masuala ya ndoa, sheria pia haijazingatia umuhimu wa elimu ya ndoa kwa wanandoa watarajiwa, haki na wajibu wa wanandoa juu ya kuhudumia watoto, mke na suala la ugawaji wa mali wakati watakapoachana.

Wizara pia imesaidia uandaaji wa rasimu ya kanuni za utaratibu katika mahakama hiyo na tayari kanuni hiyo imeshawasilishwa wizara ya Katiba na Sheria kwa hatua zaidi.

Alisema mpango huo utasaidia kupunguza ongezeko la kiwango cha talaka na athari zake katika jamii kwa mtazamo wa kijinsia na utafiti umeonesha kuwa kiwango kikubwa cha talaka hasa kwa vijana husabbishwa na mambo mbali mbali likiwemo ukosefu au elimu ndoa.

Hivyo utafiti na tathmini hizo zimependekeza kuwepo kwa sheria mahsusi inayohusiana na masuala ya ndoa.

Kuhusu makadirioya mapato na matumizi kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014, Waziri Zainab ameliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya shilingi 4,421,000,000 zikiwa ni fedha za kawaida, mishahara na kazi za maendeleo.

Nae Mwantanga Ame, anaripoti kuwa Serikali imetakiwa kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti mkubwa juu ya suala la unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume wa Zanzibar, kwani upo lakini bado haujasemwa kama unavyozungumziwa kwa upande wa wanawake.

Wazo hilo limetolewa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wakitoa michango yao katika hotuba ya Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, ukumbi wa Baraza la Wawakilishi jana.

Mwakilishi wa Kiwani Hija Hassan Hija, alisema ingawa serikali imekuwa ikifanya utafiti juu ya unyanyasaji kwa wanawake bado ina nafasi ya kuanzisha utafiti huo kwa upande wa wanaume ikiwa ni hatua ya kuweza kujua ukubwa wa tatizo hilo kwa pande zote mbili.

Alisema ni lazima serikali ione haja ya kufanya utafiti huo kutokana na hivi sasa vitendo vya unyanyasaji vinaonekana kukuwa kwa upande wa wanaume lakini bado havijawa na msemaji.

Alisema hivi sasa serikali kupitia Wizarahiyo, imeamua kuunda madawati ya kuzungumzia juu ya unyanyasaji wa kijinsia lakini kinachoonekana sehemu kubwa ya ufanyaji wa kazi zake unaonekana kuzingatia malalamiko ya wanawake pekee.

Alisema unyanyasaji huo unaonekana zaidi kwa kuharibiwa kwa watoto wa kiume ambapo hivi sasa imanza kuzoeleka kuwa ni jambo la kawaida katika mji wa Zanzibar.

Wengi wa Wajumbe wa Baraza hilo, waliochangia bajeti hiyo walionekan kukerwa na vitendo vya unyanyasaji kwa Wanawake na Watoto kwa kudai bado ni mkubwa hapa nchini kutokana na kesi zake kuendelea kutokea siku hadi siku.

Baadhi ya wajumbe hao ni pamoja ana Wawakilishi wa Wanawake akiwemo Kazija Khamis Kona, Bikame Yussuf Hamad, Amina Mabrouk, Wanu Hassan Ameir, Viwe Khamis, Asha Bakari Makame, Mwanaidi Ali, Salma Abdi, Farida Mohammed, Fatma Mbarouk Mwakilishi wa Amani na Panya Ali Abdalla.

Wajumbe wengine ambao walililamikia kuongezeka kwa unyanyasaji huo, ni pamoja na Abdalla Juma, Ismail Jussa Ladhu, Abdi Mosi, Mbwana Hamad, Jaku Hashim Ayoub, ambapo walieleza inasikitisha kuona vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake kuonekana kukuwa licha ya kuwapo kwa jitihada zinazofanywa na taasisi husika kupiga vita hilo.

Wajumbe hao walisema jambo la kusikitisha kuona sehemu kubwa ya vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha uwepo wa watoto waliotelekezwa jambo ambalo linachangia kuongeza tatizo la omba omba nchini.

Walisema hivi sasa, tatizo la omba omba limeanza kuwa ni la kutisha kutokana na idadi yake kukua kiasi ambacho kinaanza kuitia aibu Zanzibar juu ya kuwapo kwa watu wa aina hiyo.

Walisema baya zaidi kuona sehemu kubwa ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ni kundi la wanawake ambalo limekuwa likiwashirikisha na watoto katika kuifanya kazi hiyo.

Walisema hali hiyo imeonekana kuwa mbaya zaidi kwa upande wa Unguja, ambapo maeneo mengi ya omba omba hao hutumia sehemu ya Darajani, kuendesha vitendo vya aina hiyo.

Wajumbe hao, walisema baya zaidi kuona baadhi ya omba omba hao si wananchi wa Zanzibar kutokana na kuonekana huenda wakawa wanatokea Tanzania bara.

Aidha, Wajumbe hao walisema baadhi ya omba omba hao hutumia njia za kisanii kwa kujitia mimba za udanyanyifu ambazo huonekana wakati wa asubuhi lakini jioni hawanazo huku wengine wakijitia ulemavu katika miili yao.

Alisema kutokana na hali hiyo ni lazima serikali ilione tatizo hilo ukubwa wake kwani wengi wa omba omba hao hawachagui wa kuwaomba kwani huwaomba hata maskini wenzao jambo ambalo linaonesha wazi kuwa watu hao wanaifanya kazi hiyo sio kama amaskini wanaohitaji misaada bali ni watafuta fedha kwa njia za urahisi.

Walisema hilo ni kutokana na kuonekana wengi wa omba omba hao ni watu wenye nguvu za kuweza kufanya kazi za ujasiria mali na sio kuendekeza vitendo hivyo vya omba omba kwa kila siku.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya Wawakilishi hao waliiomba serikali kuona haja ya kulisimamia hilo huku serikali ikiliangalia kwa kina suala la baadhi ya wazee hao kuwatumia watoto katika kuifanya kazi hiyo, kwa kuona inaandaliwa sheria itayoweza kuwabana watu hao.

Vile vile viongozi hao waliomba kuangalia uwezekano wa kuongeza posho linalotolewa kwa wazee kwani inawezekana kuwa ni moja ya chanzo kilichosababisha kutokea kwa hali hiyo.

Walisema hilo ni lalazima kuangaliwa hivi sasa, tayari inaitia dowa nchi kwa vile sehemu kubwa ya udhalilishaji huo umeonekana hivi sasa unaweza kuiharibia Zanzibar.

Hoja nyengine ambayo ilionekana kutawala mjadala huo ni juu ya suala ala uanzishwaji wa Benki ya Wanawake ambapo walisema hawaoni sababu ni kwanini suala hilo hadi sasa halijaanzishwa wakati tayari kwa upande wa Tanzania Bara limeanza kuwafaidisha.

Aidha, Wajumbe hao waliiomba Wizara hiyo kuona misaada inayotoa kwa ajili ya kuwasaidia vikundi vya wanawake iangalie kuitoa kwa usawa kati ya Unguja ana Pemba na kufikiria kuundwa kwa Mabaraza ya vijana baada ya serikali nyingi duniani kuridhia azimio hilo.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>