Na Mwandishi wetu, DSM
AMIRI Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, amesema hakuna kijana anaekufa katika mafunzo ya kijeshi kwa sababu mafunzo wanayopewa.
Akizungumza katika sherehe za miaka 50 ya JKT zilizofanyika jana uwanja wa Uhuru, Rais Kikwete alisema, inapotokea vijana wanakufa inakuwa kwa sababu ya ugonjwa lakini si kwa sababu ya ugumu wa mafunzo wanayopewa.
Aidha Rais Kikwete aliwapongeza Wabunge 22 waliopitia mafunzo ya uongozi ya JKT, akisema walikuwa mfano bora.
Alisema Wabunge hao walikuwa na nidhamu nzuri, utii, uzalendo na moyo wa kujituma wakati wote wakiwa mafunzoni.
Alisema sasa wanaona fahari kubwa kujitambulisha kama ‘service men na service girl’ popote wawapo.
Rais Kikwete alilipongeza JKT kwa kazi kubwa iliyofanya ya kujenga uzalendo, nidhamu na ukakamavu wa vijana Watanzania.
Alisema hakuna chombo chochote cha malezi ya vijana nchini zaidi ya JKT akisema hicho ndio chombo kinachowakutanisha vijana wa dini zote, makabila yote, jinsia zote na kutoa mikoa yote na kushirikiana bila kujadili tafauti zao.
“Tunataka vijana wanaotoka hapa wawe wazalendo wa kweli na wanaotetea utaifa na kutuunganisha,” alisema Rais Kikwete.
Mafunzo ya JKT yaliasisiwa rasmi Julai 10, 1963 na kutoa vijana mbali mbali waliolitumikia taifa katika kada tafauti.
Hata hivyo, mafunzo hayo yalikufa kwa miaka mingi hali iliyosababisha maadili ya vijana kuporomoka na kukosa uzalendo hadi Machi 23 mwaka huu pale Rais Kikwete alipoanzisha upya mafunzo hayo.
Mbali na ngoma za burudani za asili, mazoezi ya kijeshi, jeshi hilo pia lilisaidia uchangiaji wa damu salama kwa lengo la kuokoa watu watakaohitaji msaada wa damu kwa dharura.
Hii ni mara ya tatu mwaka huu kwa Rais Kikwete kujumuika na jeshi la JKT katika shughuli mbali mbali.
Katika sherehe hizo, Rais Kikwete alizindua kitabu cha miaka hamsini ya kuanzishwa JKT chenye historia ya kuanazihswa jeshi hilo.