Na Maryam Salim, Pemba
POLISI Mkoa wa Kusini Pemba, limewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuvumiliana kidini na kuheshimu imani za wengine, kwa kuepuka kula hadharani katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii.
Jeshi hilo limesema limejipanga kukabiliana na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani kama vile uvaaji wa mavazi yasioendana na maadili ya kiislamu na kuhakikisha linakabiliana na uhalifu na wahalifu.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Saleh Mohammed Saleh, alitoa onyo hilo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizo ofisini kwake Madungu -Chake Chake Pemba.
“Tumejipanga vyema kufanya doria na oparesheni mbali mbali za kuwasaka wahalifu wote ili kuona wananchi wa mkoa wa Kusini wanatekeleza ibada yao kwa salama na amani,” alisema.
Aliwatanabahisha wananchi wote kuwa macho wakati wa kufutari kwani muda kama huo ni mwanya kwa wahalifu kufanya makosa kwa kuvunja nyumba na kuiba kwa vile wanajua watu wako katika harakati za futari.
Alisema katika kipindi cha Ramadhani, wahalifu hutumia mwanya huo kufanya wizi wa mazao zikiwemo karafuu, ndizi, muhogo na nazi, hivyo ni lazima wawe waangalifu na kudumisha ulinzi shirikishi katika maeneo yao.
Aidha amewataka madereva kutii sheria za barabarani, hususani nyakati za kufutari kwa kuepuka kwenda mwendo wa kasi na kupakia abiria kupindukia uwezo wa gari.