Na Joseph Ngilisho, Babati
WATU wawili wamelazwa hospitali ya wilaya Babati mkoani Manyara,baada ya kupigwa mishare ya sumu na kundi la wafugaji wa kabila la Wabarbaig waishio porini katika kijiji cha Mdorii wilayani humo.Watu hao ambao ni walinzi wa mwekezaji wa hoteli moja wilayani hapa, walikutwa na masaibu hayo walipokuwa katika shughuli zao za kawaida.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Mussa Marambo alisema tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji Mdorii, karibu na hoteli ya mwekezaji huyo aliyejatwa kwa jina la Nicholaus Negse(39) raia wa Ufaransa.
Alisema walinzi hao walikuwa katika shughuli zao za kawaida na ndipo ghafla walivamiwa na wafugaji hao ambao walikuwa wakiwavizia wanakijiji ambao siku moja kabla inasemekana waliwachoma maboma yao, ikiwa ni jitihada za kuwafukuza katika eneo hilo.
“Katika kulipa kisasi cha kuchomwa moto nyumba zao,wafugaji hao waliwachoma mishale walinzi wa mwekezaji huyo wakidhani ni miongoni mwa wanakijiji,” alisema Marambo.
Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo, walinzi hao walikimbizwa hospitali ya wilaya kwa matibabu.
Walinzi waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Ramadhani Tarimo na mwengine alitajwa kwa jina moja la moja Constantini.
Alisema watu hao wanaendelea vizuri na matibabu na hadi jana watu wawili wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Mkuu wa wilaya ya Babati,Halidi Mandiya ameamuru wafugaji hao kuhama katika eneo hilo haraka iwezekanavyo.