Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Mgogoro DRC,M23 Kukomeshwa Ndani ya Siku 17.

$
0
0
Na Kunze Mswanyama,DSM
MKUTANO wa dharura wa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGL) ulioitishwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda,umemalizika ambapo wameazimia kuhakikisha mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya serikali na kundi la waasi la M23,unamalizika ndani ya siku 17.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,alisema viongozi wa nchi hizo wamechoshwa na mgogoro huo ambapo kwa dhati wameazimia kuhakikisha unakwisha na kubakia shughuli moja tu ya kuyaangamiza makundi ya waasi.

Membe alisema,mkutano huo bado umemuidhinisha rais Museveni kuendelea kusuluhisha mgogoro huo ili kuhakikisha kundi la M23 linaweka silaha chini na kubakia kuhangaika na makundi mengine ya waasi kama Cobra,Lords Resistance Army linaloongozwa na Joseph Kony na lile la Intarahamwe.

Mkutano huo uliomalizika kwa kuwakutanisha faragha rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na Paul Kagame wa Rwanda,umefanyika siku kadhaa baada ya M23 kushambulia mji wa Goma na kuua askari mmoja wa Tanzania na wengine watano kujerehiwa.

Aidha,Membe alisema viongozi hao wamelaani vikali shambulio hilo na kulionya kundi la M23 kuwa kama halitaweka silaha chini na kumaliza mgogoro huo,litachukuliwa hatua kali zaidi.

Mgogoro huo ulianza mapema 2008.

Aliongeza kuwa,wamedhamiria kuhakikisha migogoro ndani ya maziwa makuu inatatuliwa na wenyewe kabla ya kujumuisha nchi za nje huku Umoja wa Mataifa ukitakiwa kushiriki kwa karibu zaidi kuhitimisha jambo hilo.

Pia,waliazimia kuhakikisha uchunguzi imara na wa haraka unafanyika huko Goma ili kubaini ni nani waliorusha mabomu yaliyoua na kujeruhi askari wa Tanzania hivi karibuni.

Katika hatua nyingine,Membe jana alitoa ya moyoni baada ya kusema amefurahishwa na uamuzi wa mahakama kuu ya Madagascar iliyowaondoa wagombea urais watatu ambapo walikuwa wamependekezwa na SADC kujiondoa lakini wakawa ving’ang’anizi akiwemo pia rais wa sasa Andry Rajoelina aliyeingia 2009 kwa mapinduzi ya kijeshi.

Huku akitabasamu,Membe alisema Rais Kikwete amekuwa akisuluhisha mgogoro huo kwa takribani mwaka mmoja hivyo ni furaha iliyoje kuona kuwa wamefikia malengo.

Madagascar inatarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu Oktoba mosi ambapo jumla ya wagombea 33 wanatarajiwa kugombea.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles