Na Mwantanga Ame
JESHI la Polisi limekamata watu 15 wakiwemo wengine wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi la Al-Shabab, wanaohusishwa na tukio la kumwagia tindikali Father wa Parokia ya Cheju wilaya ya kati Unguja, Anselm Mwang'amba, pamoja na lita 29 za tindikali.
Watu hao, wamekamatwa baada ya jeshi hilo kuendesha msako katika maeneo mbali mbali ya mji wa Zanzibar, ambapo baadhi yao wamedaiwa ni wafuasi wa makundi ya Al-Shabab lenye msimamo mkali wa kidini lenye maskani yake nchini Somalia.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake Kilimani mjini Zanzibar.
Alisema watu waliokamatwa wote ni raia wa Tanzania, wanaotuhumiwa kuhusika na matukio ya umwagiaji tindikali likiwemo kiongozi huyo wa dini lililotekelezwa wakati akitoka katika kituo cha huduma za mtandao wa internet cha Sun Shine kilichopo Mlandege mjinii Zanzibar.
Alisema watu hao walikamatwa katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, wakiweno watatu waliokutwa wakijitayarisha kuelekea kwenye kituo cha kundi hilo, ambapo hata hivyo kamanda huyo hakutaja kilipo kituo hicho wala majina yao.
“Tumekamata mengi, lakini hatuwezi kusema yote hivi sasa kwani tunaweza kuharibu uchunguzi wetu,” alisema.
Alisema uchunguzi wa tukio hilo umeenda sambamba na ukamataji wa tindikali ambayo imeenea Zanzibar.
Alisema tindikali hiyo, ipo iliyokamatwa madukani, nyumba za kuishi na baadhi ya ofisi, ambazo zinazifanyiwa uchunguzi.
Alisema baadhi ya wahusika wamekamatwa na tindikali iliyozimuliwa na isiyozimuliwa, na hivi sasa wanahojiwa waeleze walikoipata na kama wana vibali vya kufanya biashara hiyo ama kuingiza nchini.
Alisema polisi wameanzisha msako rasmi wa kusaka tindikali katika maeno yote ya Zanzibar, ikiwa ni hatua inayolenga kupunguza matumizi yasiyofaa nchini.
Alisema operesheni hiyo inaendeshwa na polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Jeshi la Polisi linawaomba wananchi kuunga mkono katika mapambano haya na waendelee kutupa taarifa na kutustahamilia, kwani upo uwezekano mkubwa kuwa mapambano haya yakahusu jamaa zetu,” alisema.
Akizungumzia juu ya matukio mengine ya umwagiaji wa tindikali, alisema tayari uchunguzi unaohusu raia wawili wa Uingereza, waliofanyiwa kitendo hicho katika maeneo ya Mji Mkongwe, unaendelea na watu watatu wamekamatwa kuhusishwa na tukio hilo.
Kuhusu kesi inayomuhusisha Shekh Fadhil Soraga, alisema wanasubiri matokeo ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili hatua za kuendelea na kesi hiyo ziendelee, huku akisema kesi iliyokuwa ikimuhusu aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Rashid Ali Juma, jalada lake limefungwa baada ya kukosekana ushahidi.
Aidha kesi inayomuhusu sheha wa shehia ya Tomondo, Mohammed Said Omar, alisema uchunguzi unaendelea.