Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Polisi Zanzibar yakamata bastola inayosadikiwa kutumika katika vitendo vya uhalifu

$
0
0
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi ,Zanzibar.
Jeshi la Polisi Zanzibar limefanikiwa kuwakamata watu watatu wanaosadikiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu wakiwa na bastola moja ambayo ilikuwa imefichwa katika shamba la migomba ikiwa imechimbiwa chini ya ardhi kwenye kopo la rangi.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Alli Mussa alisema watu hao walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema na ndipo walipowakamata  na katika mahojiano ya awali  watuhumiwa hao walikiri kuwa na bastola wanayoimiliki isivyo halali.
Kamanda Mussa, aliwataja watu hao kuwa ni Alli Mwanasai (40) mkazi wa Mbagala Dar es Salaam, Mohamed Said Mohamed (32) na Miraji Mohamed Rashid (40) wote wakazi wa Bububu Kigamboni  Zanzibar ambapo mpaka hivi sasa wanaendelea kuhojiwa.
“Kutokana na kukamatwa kwa bastola hii, tunaendelea kuwahoji watu hawa kwa kina zaidi ili kubaini kama matumizi ya silaha hii ilihusika katika matukio mbalimbali yaliyojitokeza hapa Zanzibar yakiwemo tukio la kuuwawa kwa Padri Mushi na kujeruhiwa  kwa Padri Ambrose Mkenda ”Alisema Kamishna Mussa.
Aidha, Kamishna Mussa alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili kujua washirika wao wengine, wakiwemo watu wanaowafadhili kwa kuwapa taarifa zinazowawezesha kufanya uhalifu, watu wanaowapa usafiri kukamilisha uhalifu huo na watu wanaowafdhili kwa pesa ili kutekeleza uhalifu huo.
Kamishna Mussa amewahakikishia wananchi kwamba kutokana na juhudi kubwa za Jeshi hilo wahalifu wote watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaowashuku kuhusika na vitendo vya uhalifu hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani  ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani baadhi ya makosa ya jinai huongezeka ikiwemo ajali za barabarani , wizi wa kuvunja nyumba usiku, vipando kuibiwa pamoja na wizi katika vituo vya mafuta hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini katika kipindi hiki na kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi pindi wanapobaini viashiria vyovyote vya  kihalifu, taarifa hizo zitalisaidia Jeshi la Polisi kudhibiti viashiria hivyo kabla uhalifu haujatendeka.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>