Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein akutana na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika

$
0
0
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Waziri wa Uingereza anayeshuhulikia masuala ya Afrika Bw. Mark Simmonds, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,leo asubuhi
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza  na Waziri wa Uingereza anayeshuhulikia masuala ya Afrika Bw.Mark Simmonds,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akifuatana  na Waziri wa Uingereza anayeshuhulikia masuala ya Afrika Bw.Mark Simmonds,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar,baada ya mazungumzo yao leo.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.}
 
Na Said Ameir,
 
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Bwana Mark Simmonds amesema dhamira ya Serikali ya nchi yake ni kuona ushirikiano uliopo kati ya Uingereza na Zanzibar unaimarishwa kwa kupanua maeneo mapya ya ushirikiano katika nyanja za Biashara na uwekezaji.
 
“Nimekuja kuthibitisha dhamira ya Serikali na wananchi wa Uingereza ya kuimarisha ushirikiano wake wa kihistoria na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kuongeza kiwango cha uwekezaji na biashara kati ya nchi zetu” alisema Bwana Simmonds.
 
Bwana Simmonds ameeleza hayo leo alipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati Waziri huyo alipomtembelea Ofisini kwake Ikulu Zanzibar.
 
Alibainisha kuwa pamoja na kutambua kuwa Uingereza inaongoza katika uwekezaji nchini Tanzania lakini nchi yake inaona kuna haja ya kuimarisha zaidi uwekezaji na biashara kwa faida ya Serikali na wananchi wa nchi mbili hizo.
 
“Uingereza ni mwekezaji mkubwa Tanzania lakini haja yetu ni kuongeza uwekezaji huo katika sekta mbalimbali ikiwemo mafuta na gesi, utalii na biashara ili kuimarisha ustawi wa watu wetu kwa kuongeza ajira pamoja na faida nyingine zitikanazo na biashara na uwekezaji”alisema.
 
Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Uingreza nchini Bibi Dianna Melrose Waziri huyo alimueleza Rais kuwa matumaini ya Serikali ya Uingereza ni kuona katika siku zijazo wawekezaji wengi wanakuja Zanzibar kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii.
 
 
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema amefurahishwa na dhamira ya Serikali ya Uingereza ya kuimarisha ushirikiano wake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar ikiwemo.
“Nimefurahishwa na jitihada za Serikali ya Uingereza ya kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania kwa kupanua maeneo zaidi ya ushirikiano katika sekta ya uwekezaji na biashara” Dk. Shein alimueleza Bwana Simmonds.
Aliongeza kuwa jitihada za pamoja za kuimairisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji kati ya Uingereza na Tanzania ni jambo muhimu sio tu kuwa kuimarisha uhusiano wetu lakini pia  kuongeza kasi ya ukuaji uchumi nchini.
“uwekezaji na biashara ni jambo muhimu kwetu Zanzibar na ningependa kuona wawekezaji zaidi kutoka Uingereza wanakuja Zanzibar kuwekeza katika sekta mbali mbali  kama uvuvi wa bahari kuu na Utalii” alibainisha Dk. Shein.
Alifafanua kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ingawa hivi sasa Zanzibar imeweza kuvutia wawekezaji wa hoteli ya hadhi ya juu kwa mfano wa nyota tano lakini bado inahitaji uwekezaji zaidi wa aina hiyo ili kuimarisha sekta hiyo kuvutia watalii wengi zaidi na wa hadhi ya juu.
Dk. Shein alimueleza waziri huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatilia mkazo pia uwekezaji katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu ambayo hadi sasa haijapata wawekezaji, hivyo alisema ni matumaini yake kuwa wawekezaji kutoka UingEreza watatumia fursa hiyo kuja Zanzibar.
“Ni sekta ambayo ikitumika vyema itabadili maisha ya watu wetu wengi. Tumeunda Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu na imeanza kazi hivyo matumaini yetu wawekezaji kutoka Uingereza wataitumia fursa hiyo kuwekeza”alieleza.
Dk Shein alitumia fursa ya mazungumzo hayo kuishukuru serikali ya Uingereza kwa misaada yake kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar imekuwa ikifaidika na misaada hiyo.
Miongoni mwa waliohudhuria mazungumzo hayo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame na Katibu Mkuu Kiongozki Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>