Na Masanja Mabula, Pemba
BAADHI wananchi wa Shehia ya Ukunjwi Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wamegomea mazishi ya marehemu aliyekuwa anaishi ya VVU.Taarifa ambazo zimepatikana na mwandishi wa habari hizi zinasema kuwa mazishi hayo ya marehemu Fatma Suleiman Ngasa (Chausiku) yalichelewa kufanyika kutokana na wananchi kutofautiana na kila upande ukisusa kutokana na kuhofu kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Chanzo chetu cha habari kinasema wanachama wa ZAPHA+ Wilaya ya Wete walilazimika kuchukua gari kwenda kumstiri mwenzao, baada ya kupata taarifa kwamba wananchi wa Shehia hiyo wameendesha mgomo baridi .
Aidha chenzo chetu kimezidi kufahamisha hata suala la dini nalo lilichukua nafasi yake, licha ya marehemu huyo kuwa ni muumini wa dini ya Kiislamu, lakini baadhi ya wananchi walionekana kupingana na maelezo yaliyotolewa na ndugu wa marehemu.
"Unajua bado jamii inashindwa kuelewa njia za maambukizi, hali hiyo ndiyo iliyopelekea kuchelewa kufanyika kwa mazishi wa marehemu , lakini tunashukuru sana uongozi wa Sheha kwa kulisimamia hadi mazishi kufanyika, " kilifahamisha chanzo chetu cha habari .
Aidha habari za uhakika ambazo zimepatikana na mwandishi wa habari hizi zinasema msukumo wa kufanyika kwa mazishi hayo pia ulichangiwa na wanachama wa ZAPHA+ ambao walishirikiana na sheha kuona mwili wa marehemu unahifadhiwa katika makaazi yake ya kudumu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Sheha wa Shehia ya Ukunjwi, Mkongwe Kasanje amesema hali ya mabishano iliyokuwepo wakati wa mazishi wa hayo iliepelekea kuchelewa kwa muda shughuli za kuustiri mwili wa marehemu.
Sheha huyo aliishangaa jamii kuona inashindwa kutambua njia za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi , licha ya elimu ya Ukimwi kuendelea kutolewa siku hadi siku.
" Mimi naamini jamii jamii imeshapata elimu ya Ukimwi , lakini hii imenipa wasi wasi wa kwamba bado elimu zaidi inahitaji kutolewa ili jamii iweze kutambua kwamba unyanyapaa wa watu wanaoishi na VVU hauna nafasi katika jamii ya leo," alifahamisha.