Na Mwajuma Juma
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa itafanya kila liwezekano ili kuhakikisha uwanja wa Amaan unakamilika kama ulivyopangwa.
Kauli hiyo ameitowa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika ziara ya kukaguwa uwanja huo jana ambao umeanza matengenezo ya kutaka kulazwa nyasi bandia Septemba mwaka huu.
Alisema kuwa wakati wakarandasi wakiwa katika hatua za matengenezo wasisite kutoa taarifa yoyote kwa Serikali juu ya kutaka msaada kama itatoke3a kufanya hivyo.
“Kama kutakuwa na hali yoyote ile ya kutaka kusaidiwa basi tupo tayari kusaidia na msisite kutoa taarifa kwetu”, alisema.
Aidha aliupongeza uongozi wa uwanja huo kwa mipango mizuri ya kuuendeleza uwanja huo na kusema kuwa wanakabiliwa na kazi ngumu na kubwa katika mipango yao hayo hadi kufanikisha kwake.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii, Utamaduni na Michezo Ali Mwinyikai alisema kuwa kazi ya kulaza nyasi bandia ilikuwa ianze wiki ijayo lakini itashindikana baada ya kuchelewa kwa baadhi ya vifaa ikiwemo gundi.
Alisema kuwa vifaa hivyo vilipaswa kufika jana lakini kwa sasa vinatarajiwa kuwasili Disemba 5 mwaka huu, huku ujenzi huo ukitarajiwa kukamilika Disemba 15 mwaka huu.