Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk. Shein aipongeza UNICEF kwa kusaidia Zanzibar. Atuma rambirambi vifo vya wanajeshi Darfur

$
0
0
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto (UNICEF), kwa juhudi zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo alipozungumza na Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Dk. Jama Gulaid, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumtambulisha Francesca Moranditi atakayefanya kazi za Shirika hilo katika ofisi ya Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Shirika hilo limekuwa na historia kubwa kwa mashirikiano na Zanzibar.

Alisema UNICEF imeweza kushirikiana vyema na Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo pamoja na huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya, elimu na kuwasaidia kuwajengea uwezo akina mama na watoto.

Alisema Shirika hilo limeweza kutoa msaada wake mkubwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kuimarisha sekta ya fya nchini.

Alisisitiza kuwa Zanzibar imeweza kujiweka katika nafasi nzuri kufikia malengo ya milenia katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya kwa kuweza kuungwa mkono na washirika wa maendeleo likiwemo UNICEF.

Aidha, alisema kupungua vifo vya akina mama na watoto nchini ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alitumia fursa hiyo kumkaribisha Morandini Zanzibar na kumuhakikishia mashirikiano makubwa atayapata kutoka kwa viongozi wa Serikali na wananchi wa Zanzibar kutokana na ukarimu wao na utamaduni wao wa kupenda wageni.

Mapema katika mazungumzo yake, Dk. Jama Gulaid alimueleza Dk. Shein kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta zake za maendeleo na kutoa pongezi zake kwa kuendelea kuwaenzi na kuwatunza watoto.

Alisema mbali na juhudi hizo Zanzibar imeweza kupata mafanikio katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto pamoja na kupambana na malaria hatua ambayo imeipa sifa Zanzibar ndani na nje ya Afrika.

Alisema mabadiliko makubwa yameweza kutokea katika kuhakisha watoto wanapata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu juhudi ambazo zinaendelea kufanywa na serikali.

Alimuhakikishia Dk. Shein kuwa shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano wake na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ili iweze kupata mafanikio zaidi.

Sambamba na hayo, Dk. Gulaid alimueleza Dk. Shein kuwa UNICEF itandelea kuwajengea uwezo wafanyakazi wake pamoja na kuziimarisha ofisi zake zote zilizopo Tanzania ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Nae Francesca Morandini alitoa pongezi na shukurani kwa Dk. Shein kutokana na kumkaribisha Zanzibar na kumuahidi kuwa UNICEF inathamini na kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hasa katika kuwajali watoto.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameelezea kupokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za vifo vya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa wakati wakilinda amani katika mji wa Darfur nchini Sudan.

Dk. Shein alisema inasikitisha zaidi kuwa wanajeshi hao wamekufa wakiwa katika kazi ya kulinda amani nchini humo na kueleza kuwa wao ni mashujaa na wamekufa kishujaa.

Dk. Shein alituma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange na wanajeshi wote na kuzitakia pole familia za wafiwa.

Katika salamu hizo, Dk. Shein alisema mauaji hayo ni msiba wa Taifa lote na wananchi wote wa Zanzibar wanaungana pamoja katika kuomboleza msiba huo.

“Tunatoa pole na tunamuomba Mwenyezi Mungu aziweke pahala pema peponi roho za mashujaa hao, vile vile tunawatakia nafuu ya haraka majeruhi wote,” alisema Dk. Shein.

“Mwenyezi Mungu akupeni moyo wa subira na ustahamilivu katika kipindi hiki cha msiba mkubwa,” aliongeza katika salamu hizo.

Alisema yeye binafsi pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wenzao kuwaombea wale wote waliojeruhiwa katika tukio hilo ili waweze kupona kwa haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani.

Wanajeshi saba wa JWTZ waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa Sudan na wengine kujeruhiwa.




Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>