Na Mwandishi wetu
MIILI ya wanajeshi wa Tanzania waliouawa katika jimbo Nyala katika mji wa Darfur nchini Sudan, itafanyiwa uchunguzi na Umoja wa Mataifa kabla ya kurejeshwa nyumbani kwa taratibu za mazishi.
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe, alisema baada ya uchunguzi utakaofanyika mjini Khartoum, Sudan, Umoja wa Mataifa utatoa ndege ya kuisafirisha miili hiyo Tanzania.
Alisema kwa sasa miili ya wanajeshi hao ipo mjini Khartoum.
Kanali Mgawe alisema baada ya kurejeshwa nyumbani, miili ya wanajeshi hao itahifadhiwa hospitali ya jeshi Lugalo na siku inayofuata itapelekwa katika viwanja wizara ya ulinzi kwa ajili ya kuagwa.
Alisema baadae miili ya wanajeshi hao itasafirishwa kwenda katika maeneo wanakotokea kwa shughuli za mazishi.
Akizungumzia hali za majeruhi, alisema wanajeshi tisa tisa waliolazwa katika hospitali ya Nyala hali zao zinaendelea vizuri.
Hata hivyo, alisema wanne wako chini ya uangalizi maalum wa madaktari.
Aidha alisema mmoja amehamishiwa mjini Khartoum kwa matibabu zaidi na kwamba afya yake ndio inalitia hofu jeshi.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limelaani vikali shambulio lililofanywa dhidi ya walinda amani wa Tanzania katika jimbo la Darfur na limetaka uchunguzi wa kina ufanyike.
Taarifa ya Baraza hilo ambalo ndilo lenye dhamana kuu ya usimamizi wa amani ya kimataifa na jukumu la kuidhinisha misheni zote za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, imetolewa kwa niaba ya Baraza na Marekani ambaye ni Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Julai.
Taarifa inasema, wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama wanalaani kwa nguvu zao zote mashambulizi yaliyofanyika Julai 13 na watu wasiojulikana dhidi ya walinzi wa amani wa UNAMID huko Darfur, waliokuwa katika doria magharibi ya Nyala kusini mwa Darfur na kusababisha vifo vya walinzi wa amani saba , majeruhi 17, akiwamo polisi huku hali za majeruhi wawili kati yao ikielezwa kuwa ni mbaya.
Walitoa salamu zao za rambirambi kwa familia za walinzi hao waliopoteza maisha katika shambulizi, kwa serikali ya Tanzania na UNAMID.
Limeitaka serikali ya Sudan kufanya uchunguzi wa kina juu na tukio hilo na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wale wote waliohusika.
Taarifa hiyo inaeleza zaidi kwamba Baraza Kuu la Usalama , limeonyesha wasiwasi wake kuhusu mazingira ya shambulio hilo, moja ya shambulio baya kuwahi kufanyika dhidi ya walinzi wa UNAMID tangu kuanzishwa kwake.
Katika taarifa yake hiyo limesisitiza kwamba shambulio au vitisho vya aina yoyote dhidi ya UNAMID havikubaliki na limetaka kutojirudia tena kwa tukio kama hilo.
Pia Baraza Kuu la Usalama limerejea msimamo wake kwamba linaunga mkono kwa kauli moja misheni ya kulinda amani ya UNAMID na limetoa wito kwa pande zote huko Darfur kushirikiana na misheni hiyo.
Wakati huo huo, kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, amekuwa akipokea kwa niaba ya serikali na familia, salamu za pole kutoka kwa mabalozi wenzake.
Miili ya wanajeshi waliouawa inatarajiwa kurejeshwa nyumbani kesho kwa taratibu za mazishi.