Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Mabaraza yaanza kuifumua rasimu ya katiba.

$
0
0
 Wataka Rais kwa awamu
 
Makamu awe Rais wa upande mmoja
 
Na Haroub Hussein
WAJUMBE wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Kati wametaka katiba mpya ieleze utaratibu wa kupatikana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uwe kwa awamu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Wajumbe hao walisema ili kuondosha kero iliyopo sasa ya kupatikana Rais katiba hiyo ieleze moja kwa moja endapo awamu ya kwanza Rais atatoka Tanzania Bara awamu inayofuata atoke Zanzibar.

Wakitoa maoni yao katika kikao cha Baraza la Katiba la Wilaya hiyo lililofanyika katika skuli ya Dunga, wajumbe hao walisema utaratibu huo mpya utaondosha malalamiko yaliopo sasa ambapo Rais anapatikana bila ya kuzingatia pande mbili za Muungano.

Pia wajumbe hao wametaka Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe Rais wa Zanzibar huku wakitaka suala la mafuta na gesi kubaki kuwa la muungano.

Kuhusu suala la elimu ya juu, wametaka liendelee kubaki kuwa la muungano kwa vile nchi washirika hazina mamlaka ya uhusiano wa kimataifa.

Aidha wametaka kipengele cha mgombea binafsi kiondolewe kwa vile mgombea huyo hatokuaa na mdhamini wala mtu wa kumdhibiti pale atapokwenda kinyume na maadili ikilinganishwa na utaratibu wa sasa ambapo wagombea wanatoka katika vyama vya siasa, hivyo wanapokwenda kinyume na maadili ya vyama hivyo wanaadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za vyama.

Aidha wametaka umri wa Rais uliopendekezwa wa miaka 40 ufutwe na uwe miaka 25 ili vijana ambao ndio wengi katika jamii waweze kupata fursa ya kugombea nafasi hiyo.

Aidha wametaka utaratibu wa Spika kuwa asiwe na chama ufutwe wakisema ni mgumu kutekelezeka kwa vile hakuna mtu asie na chama.

Walisema matokeo ya rais yakubaliwe hata ikiwa mgombea kashinda kwa kura moja bila ya kuangaliwa asilimia hamsini, kwani hilo litaepusha gharama zisizo za lazima za kurudia uchaguzi.

Katika baraza hilo wajumbe wengine wametaka utaratibu wa kuwepo serikali tatu upite kama ilivyopendekezwa na ili kuondosha kero zilizopo sasa za kuwa upande mmoja wa muungano hauna serikali.

Akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa baraza hilo, waliotaka kujua rasimu hiyo ilipatikana vipi, Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Assaa Rashid alisema tume hiyo awali ilipita kukusanya maoni ya watu wa makundi mbali mbali baada ya kumaliza mchakato huo ndipo ilipopendekeza rasimu hiyo ya kwanza ya katiba pamoja na kuendelea na hatua zinazofuata.

Akifunga Baraza hilo, Mwenyekiti wa kikao hicho, Awadh Ali Said ambae ni Mjumbe wa Tume hiyo, alisema maoni yote yaliyotolewa katika baraza hilo yatawasilishwa tume kwa kufanyiwa kazi.

Awadh alisema michango iliyotolewa imeweza kuisaidia tume kupata mambo mengine mapya ambapo awali hayakuwepo.

Alisema tume inawashukuru wajumbe hao kwa kutoa maoni yao kwa uhuru na kuheshimiana sambamba na kuvumiliana wakati wote wa baraza hilo.

Aliwambia wajumbe hao kuelewa kuwa hakuna katiba inayoridhisha na watu wote lakini lazima iguse maeneo yote muhimu.

Tume ya Mabadiliko ya katiba imemaliza mikutano yake kwa baraza la katiba la Wilaya ya kati kwa upande wa Zanzibar na leo inaendelea na vikao vyake katika baraza la wilaya ya Kaskazini “A” katika kituo cha mafunzo ya amali Mkokotoni.




Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>