Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF huko Buguruni, kulia ni Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Masoud
Mwenyekiti Limba na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakiingia ukumbuni Buguruni
Khamis Haji OMKR
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema nchi inakumbwa na msukosuko mkubwa wa kiuongozi na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete anapaswa kuchukua maamuzi ya busara ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa hivi sasa, ili kulinusuru Taifa.
Profesa Lipumba amesema hayo leo (21/12/2013) wakati alipokuwa akifungua mkutano wa Kawaida wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, unaofanyika Makao Makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.
Amesema msukosuko huo unaonekana wazi kufuatia taarifa ya Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, Hali ya kukosekana kwa uwazi katika Mchakato wa katiba na Hatma ya Uchaguzi Mkuu 2015, pamoja na malalamiko ndani ya CCM kwamba kuna Mawaziri wengi ndani ya Serikali ni mizigo.
Mwenyekiti Lipumba amesema hali iliyopo inaonesha Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Kikwete hivi sasa imekosa kusimamia uadilifu na Utawala bora na kwamba ni vigumu kuweza kusimamia haki na utawala bora kwa wananchi wake.
Amesema maamuzi ya busara yatakayoweza kuinusuru hali hiyo ni kwa Rais Kikwete kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoweza kuleta maridhiano na kuiepusha nchi na madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na hali iliyopo sasa.
Amesema ripoti ya Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyotolewa juzi Bungeni na kusababisha Mawaziri wanne kupoteza nyadhifa zao, inathbitisha hali si shwari na kwamba nchi imekumbwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu na kukosekana utawala bora.
Amesema watu waliokwenda kutokomeza ujangili, badala yake wamekuwa wavunjaji wakuu wa haki za binaadamu kwa kutesa watu wasiokuwa na hatia na kusababisha baadhi ya watu hao kupoteza maisha na mali nyingi za wananchi wakiwemo wafugaji kupotea.
Profesa Lipumba amesema vitendo kama hivyo imekuwa ni vya kawaida kufanya hapa nchini na vinahusisha zaidi watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo katika opresheni za kijeshi zinazoendeshwa mara kwa mara, kama ambavyo pia ilitokea mkoani Mtwara.
“Kuachishwa kazi Mawaziri wanne, huku Katibu Mkuu wa CCM akilalamika kuwepo Mawaziri wengine ambao ni mzigo, kuna maanisha kuna msukosuko mkubwa ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwamba hivi sasa hali ni mbaya sana”, amesema Mwenyekiti Lipumba.
Akizungumzia mchakato wa Katiba na hatma ya uchaguzi mkuu ujao, amesema, wakati inaonesha wazi Katiba Mpya haitaweza kupatikana katika muda uliopangwa awali ifikapo mwezi April mwakani, bado wananchi hawaelewi utaratibu gani utatumika kuwawezesha kupiga kura ya maoni na kushiriki katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Amesema tangu mwaka 2010 ulipofanyika uchaguzi mkuu daftari la wapiga kura halijafanyiwa mapitio, wakati utafiti unaonesha katika kipindi hicho hadi sasa kuna Watanzania wapatao milioni nne watakuwa wametimiza miaka 18 na kuwa na haki ya kupiga kura.
Amesema wakati daftari hilo halijafanyiwa mapitio nao mpango wa Serikali wa kuwapatia wananchi vitambulisho vya uraia, ambavyo vilieleza vingetumika kupigia kura unakwenda kwa kusuasua na kwamba hadi sasa hakuna mkoa hata mmoja uliokamilisha kuwapatia wananchi wake vitambulisho hivyo.
“Mambo haya yako katika hali ngumu, hatuwezi kuingia katika uchaguzi mkuu 2015 na katiba ambayo wananchi wengi wameshapoteza imani nayo. Ni vyema Rais Kikwete aunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa hivi sasa”, amesema Profesa Lipumba.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kikao hicho kitajadili ajenda zipatazo 13 zote zikiwa na maslahi kwa chama hicho pamoja na Taifa.
Amesema jumla wajumbe 40 wa Baraza Kuu la JUongozi la CUF wanahudhuria kikao hicho, kati ya wajumbe wote 54, na hivyo kikao hicho maamuzi yatakayoweza kufikiwa ni halali.
Aidha, Maalim Seif alitangaza kwamba chama kimepata msiba mkubwa kufuatia kifo cha mjumbe wa Baraza Kuu, Zainab Nyumba kutoka Mwanza ambaye alifariki juzi baada ya kuugua Malaria na alitarajiwa kuzikwa jana huko Mkoani Mwanza.