Na Himid Choko, BLW
Katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Ndugu Yahya Khamis Hamadi amewataka Wajumbe wa Baraza hilo kutimiza wajibu wao wa kikatiba kwa kuidhibiti Serikali ili kuendeleza uwajibikaji.
Amesema hatua hiyo itafikiwa kwa kuihoji kuhusiana na sera , mipango maalum ya kibajeti pamoja na kuiuliza masuala mbali mbali yanayohusu uendeshaji , utekelezaji na usimamizi wa shughuli zake.
Ndugu Yahaya amesema hayo leo Wakati akitoa mada kuhusiana na Dhana ya Baraza la Wawakilishi katika kuisimamia serikali iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza hilo Mbweni kwenye semina ya siku moja iliyowashirikisha wajumbe wa Baraza hilo.
Amesema Kanuni za Baraza hilo zimeelekeza wazi Utaratibu wa Mawaziri kuulizwa maswali kuhusu jambo lolote la Umma au jambo jengine ambalo linasimamiwa na wizara zao. Amesema Mjumbe pia anaweza kuuliza suala Kwa jambo ambalo Baraza limemteuwa kulishughulikia .
Amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni serikali ya wananchi, hivyo wananchi hao kupitia wawakilishi wao waliowatuma kuwawakilish wana haki ya kupata taarifa juu ya mambo yanavyoendeshwa katika serikali yao .
Katibu huyo wa Baraza la Wawakilishi amezitaja mbinu nyengine za kuidhibiti serikali kua ni pamoja na utungaji wa Sheria ambazo itazifuata katika utendaji wa shughuli na mwenendo wake.
Amesema hatua hii ya utungaji wa sheria itasaidia kwa mtu au kikundi chochote cha watu kuweza kwenda mahakamani kupinga kitendo au uamuzi uliofanywa na serikali kinyume na sheria.
Ameongeza kufahamisha kwamba njia nyengine ya kudhibiti utendaji wa serikali ni uidhinishaji wa Bajeti kwa sababu idhini ya Baraza inahitajika ili serikali iweze kutumia fedha za wananchi katika kutekeleza mipango yake.
“ Endapo Baraza halikuridhishwa na mpango fulani unaokusudiwa kutekelezwa na serikali au halikuridhika na fedha zilizoombwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo , basi linaweza kuukataa mpango huo “ Alisisitiza ndugu Yahya.
Hata hivyo Katibu huyo wa Baraza la Wawakiklishi amesema kwa namna Baraza hilo linavyofanya kazi hivi sasa na bila ya Wajumbe wake kujidhatiti, basi serikali itachukua muda kurekebisha baadhi ya Mapungufu yanayoibuliwa na Baraza hilo na kufanyakazi bila ya kusimamiwa.
Amewataka wajumbe hao kufanya kazi zao kwa umakini mkubwa hasa wanapokua katika Shughuli za Baraza na Kamati zake ili kulinda hadhi na heshima kubwa ya chombo hicho.
Kwa upande wa wajumbe hao wameelezea wasi wasi wao mkubwa hasa kwa Utaratibu wa hivi sasa wa kupitisha kwanza Bajeti ya serikali kuu na kufutiwa na bajeti za kisekta.
Wamesema Utaratibu huo unawafanya kukosa nguvu za kuhoji au kuikataa Bajeti za Kisekta kwa vike inakuwa tayari zimeshapitishwa katika bajeti kuu.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais , Ikuli Mheshimiwa Dr. Mwinyi Haji Mwadini amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbali kutokana na Ripoti au maagizo mbali mbali yayotolewa na Baraza la Wawakilishi.
Akitowa mfano Dr. Mwinyi Haji amesema katika Ripoti ya Baraza la Wawakilishi inayotokana na Kulichunnguza Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO ) na Baraza la Manispaa Serikali iliwaita wahusika wakuu na kuwahoji pamoja na kuchukua hatua mbai mbali kwa waliobainika na na kasoro mbali mbali.
Semina hiyo iliyofunguliwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho imedhaminiwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP chini ya |mapango wake wa Kusaidia Mabunge na Vyombo vya Kutunga sheria.