Na Amina Omari,Tanga
WATU sita wamefariki dunia papo hapo na wengine 26 kujeruhiwa baada ya daladala kuligonga lori la mizigo, katika eneo la Kange barabara kuu itokayo Tanga mjini kwenda Muheza.
Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana na ilihusisha gari la abiria lenye namba za usajili T909 ATV lililokuwa likiendeshwa na Gadiel Elikaeli na lori la mizigo aina ya Volvo lenye namba za usajili T260 DYM.
Alisema chanzo cha ajali ni mwendo kasi baada ya dereva wa daladala ambaye alifariki kutaka kulipita gari jingine bila kuchukua tahadhari na kujikuta anajiingiza kwenye lori lililokuwa limeharibika.
Aliwataja waliofariki kuwa ni Raymond Mapunga (28),Halima Shaka (28),Marrya Chilongoi (37),Glory Kidenya (1),Femida John (38) na dereva wa basi hilo Gadieli Elikaeli (44) wote wakazi wa Kange.
Hata hivyo, alisema majeruhi 21 walipelekwa hospitali ya rufaa ya Bombo kwa matibabu zaidi huku majeruhi wanne wakitibiwa katika hospitali ya wilaya na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Nae Muuguzi wa zamu katika hospitali ya rufaa ya Bombo, Alice Mkande alisema walipokea majeruhi 21 kati yao 6 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa ambapo majeruhi 17 wanaendelea na matibabu.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Charles Kiluwa, alisema ajali hiyo ingeweza kuepukika kama dereva wa daladala angekuwa makini.