Na Khamis Amani
WATU wasiojulikana wamevamia ofisi za kampuni ya ushauri ya a Imara Consultant kuiba kasha la kuhidhia fedha ndani yake mkiwa na mamilioni ya shilingi na fedha za kigeni.
Watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za jadi, walivamia ofisi hizo zilizopo Vuga mjini Unguja baada ya kumuweka chini ya ulinzi mlinzi aliyekuwa amelala juu ya meza.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mkadam Khamis Mkadam alisema, tukio hilo lilitokea kati ya saa 2:00 usiku na saa 11:00 ya alfajiri ya Disemba 13 mwaka huu.
Akizungumzia tukio hilo , alisema kabla ya wizi huo, watu hao walivunja geti la nje na mlango wa ndani wa kuingilia ndani ya ofisi hiyo na kuchukua kasha la fedha na kuondoka nalo.
Fedha zilizokuwemo ni shilingi 1,200,000, dola 22,000 za Marekani 22,000 Euro 3,000 pamoja na riale za Oman ambazo idadi yake hazijajulikana.
Alisema kasha hilo lilionekana limetupwa maeneo ya skuli ya Dimani na kwamba Polisi wanaendelea na uchunguzi na kuwasaka wahusika.
Aidha alisema Polisi wameokota maiti ya mtoto mdogo wa kike wa miaka mitano, ikiwa kwenye migomba.
Alisema, maiti hiyo ni ya Iklima Ali Mohammed mkaazi wa Magogoni aliyefariki dunia baada ya kukokotwa na maji ya mvua.
Tukio hilo lilitokea Disemba 16 mwaka huu saa 7:30 mchana na uchunguzi wa daktari ulionesha alifariki baada kukosa pumzi.
Aidha amewataka wananchi kusherehekea sikukuu ya krismasi kwa amani na utulivu, akisema polisi wamejiimarisha kudhibiti vitisho vyovyote vya uhalifu.
Alisema polisi wameimarisha doria za magari, miguu, pikipiki na mbwa kuhakikisha watu wanasherehekea sikukuu kwa utulivu.