Na Khamisuu Abdallah
MKUTANO mkuu wa tatu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita umeshindwa kuwapata viongozi wanne wa kitaifa, kutokana na utata wa kikatiba.
Mkutano huo uliofanyika ukumbi wa sanaa Rahaleo, pamoja na mambo mengine uliambatana na uchaguzi mkuu wa viongozi wa kuliongoza Shirikisho hilo kwa miaka mitano ijayo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi Mohammed, alisema nafasi zilizoshindwa kujazwa ni Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti, Mwenyekiti wa wanawake na Mwenyekiti wa vijana.
Alisema sababu zilizosababisha nafasi hizo kushindwa kujazwa ni pamoja na utata wa kikatiba, ambapo mshindi anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Alisema wagombea wote wameshindwa kufikia kiwango hicho na katiba haikutoa maelezo yoyote kuhusu hatua za kuchukua.
“Hakuna mizengwe iliyotokea kama watu wanavyosema, uchaguzi lazima uendeshwe kwa kwa kanuni na kanuni yetu inaelekeza hivyo, hichi ndicho kilichosababisha kushindikana kupatikana viongozi,” alisema.
Alisema ZATUC italazimika kuitisha uchaguzi katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu ijayo.
Alisema baraza kuu la ZATUC limemteua Zaharan Mohammed Nassor kuwa Kaimu Mwenyekiti hadi uchaguzi utakapofanyika.
Aidha aliwataka wanachama kutumia busara pale kunapojitokeza tatizo ili kuepusha migogoro.