Na Mandishi Wetu
USHIRIKIANO wa pamoja unahitajika baina ya jeshi la Polisi Zanzibar na wadau wa utalii ili kukomesha vitendo vya uhalifu dhidi ya watalii.
Akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya wawekezaji wa sekta ya utalii Zanzibar (ZATI) na Jumuiya ya watembeza watalii (ZATO) ofisini kwake Ziwani mjini Unguja, Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Hamdan Omar Makame, alisema sekta ya utalii inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhalifu.
Alisema utalii una mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi hivyo ni lazima wadau wote wajipange ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.
“Asilimia 80 ya mapato ya serikali yanatokana na utalii,” alisema.
Alisema kukiwa na ushirikiano wa dhati baina ya taasisii hizo na jeshi la polisi kutapunguza mwanya kwa wahalifu kushambulia watalii.
“Tafadhalini msinipe nafasi ya kupumzika, wakati matukio yapo nipigieni simu hata usiku wa manane, tukio la uhalifu likitokea saa mblili usiku lisifikishwe asubuhi, toeni taarifa mapema kabla halijaathiri nami nakuhakikishieni polisi watafika mapema kwenye eneo la tukio”, alisema.
Alitumia fursa hiyo kuziomba taasisi hizo kulisaidia jeshi la polisi vifaa vya kisasa vinavyoendana na teknolojia iliopo zikiwemo radio za digitali na kamera zitakazoliwezesha kumuona askari akiwa katika eneo lake la kazi alilopangiwa.
Aidha aliwataka kuweka kamera maalum kwenye magari yanayobeba watalii ambazo zitanasa matukio yote yanayofanywa dhidi ya watalii.
Aliwahimzwa wamiliki wa mahoteli kuweka kamera za usalama (CCTV) ndani na nje ya hoteli ili kunasa picha za wahalifu.
Akizungumzia sababu zinazochangia uvunjifu wa amani hasa katika sekta ya utalii, alisema ukosefu wa ajira kwa vijana huchangia vitendo vya uhalifu.
Nae Kamishna wa Kamisheni ya Utalii kutoka sekta binafsi, Hassan Ali Mzee, alisema kamisheni ina uhisiano mzuri wa kidipolomasia na balozi zote ambazo nchi zao zinaleta watalii.
Alisema uhalifu unapotokea Kamisheni inapata picha mbaya kutoka ofisi za kibalozi, hivyo aliliomba jeshi la polisi kuunda kikosi kazi kitakachopewa nguvu ya kudhibiti uhalifu dhidi ya watalii.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya watembeza watalii, Khalifa Mohammed Makame, alisema usalama ni uhai kwa sekta ya utalii na kuviomba vyombo vya usalama likiwemo jeshi la polisi kushirikiana na sekta binafisi hasa watembeza watalii.
Mwenyekiti wa bodi ZATO, Naila Jidawi, alisema vitendo vya uhalifu vinachangia kupunguza idadi ya watalii.