Na Kadama Malunde, Shinyanga
SIKU chache baada ya mtoto mmoja kubakwa, kuuawa kisha mwili wake kuwekwa kwenye boksi na kutupwa karibu na jaa kuu la Ngokolo Mitumbani manispaa ya Shinyanga, mtoto mwingine aitwaye Jamila Ramadhani (4) ameuawa kikatili baada ya kupigwa kipande cha bomba ya maji kichwani na mama yake wa kambo.
Tukio hilo limetokea eneo la Mshikamano katika manispaa ya Shinyanga ambapo baada ya tukio mama hiyo amekimbia.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla alisema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 12:37.
Alisema mama huyo wa kambo aitwae Moshi Kasema (35) alimpiga mtoto huyo sehemu ya kichwa baada ya mtoto huyo kujisaidia bila kujisafisha,kitendo ambacho kilimkera.
Alisema wakati mauaji hayo yakifanyika baba wa mtoto huyo, Ramadhani Faustine hakuwepo nyumbani na kuongeza kuwa mama mzazi wa mtoto huyo alishafariki dunia.
Polisi wanamtafuta mwanamke huyo ili afikishwe katika vyombo vya sheria.