Na Rose Chapewa, Kilombero
MRATIBU wa huduma za macho mkoa wa Morogoro, Dk. Sencord Njau amesema inakadiriwa watu 22,188 wana tatizo la upofu katika mkoa wa Morogoro na kwamba kati yao 11,094 tatizo hilo limesababishwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho ambao unaweza kutibika.
Mratibu huyo alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kampeni maalum ya matibabu ya mtoto wa jicho inayoendelea katika kituo cha afya cha Mlimba wilayani Kilombero mkoni hapa.
Dk. Njau alisema kutokana na hali hiyo, ndio maana wameanza kampeni maalum ya matibabu ya macho, inayohusisha pia upasuaji,katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro.
Alisema kampeni hiyo inayoendeshwa na Idara ya Afya Mkoa wa Morogoro, chini ya ufadhili wa Shirika la Sight Savers Tanzania na shirika la kimataifa la kusaidia jamii la nchini Uturuki, IHH, imeshatolewa bure kwa wananchi wa wilaya ya Kilosa katika kampeni maalum iliyoendeshwa katika kituo cha afya Kimamba.
Alisema katika kampeni hiyo, wamelenga kufanya upasuaji kwa watu 300, katika wilaya za Kilosa, Kilombero na Mvomero ambapo kati ya idadi hiyo, watu 11,000 wanahitaji huduma hiyo.
“Mnaweza kuona ni idadi ndogo sana ikilinganishwa na mahitaji, lakini tunalenga watu hao kwa awamu, kama awamu hii ni 300, awamu nyingine tutaongeza kufikia 500 na kuendelea hivyo hivyo hadi kuhakikisha tatizo hili limekwisha kama sio kupungua kabisa,” alisema.
Alisema tatizo hilo la mtoto wa jicho limekuwa likiwaathiri watu wengi wakiwemo wazee na watoto wadogo hata kabla ya kuzaliwa na kwamba
katika kampeni zinazoendelea ambazo Kilombero zimeanza katika kituo cha afya Mlimba huku Mvomero wakitegemea kutoa huduma hiyo katika hospitali ya Turiani, wamewalenga zaidi watu wazima.
Kwa upande wake Afisa Muuguzi wa macho mkoa wa Morogoro, Ernold Mligo alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa tatizo la mtoto wa jicho lina tiba, hivyo ni vyema wakawahi katika vituo vya afya, hospitali na maeneo mengine ya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka.