Na Kadama Malunde, Shinyanga
MAMIA ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga wamejitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Zuhura Mashaka aliyefariki ghafla alipokwenda kutafuta kazi katika mgodi wa madini Geita (GGM) mkoani Geita,siku chache tu baada ya kuhitimu masomo yake ambapo mazishi yamefanyika katika kijiji alichozaliwa cha Kituli, kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga.
Mazishi ya marehemu Zuhura (23) aliyekuwa anasomea shahada ya elimu ya miamba madini yamefanyika jana na kuhudhuriwa na watu wa kada mbalimbali wakiongozwa na Mbunge wa viti maalum, Azza Hilal.
Akitoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, Mbunge huyo alisema kijana huyo ambaye ndio kwanza alikuwa amehitimu masomo na kuanza maisha alikuwa tegemeo hivyo ameacha pengo kubwa sio tu kwa familia au kijiji chake bali taifa kwa ujumla.
“Zuhura alikuwa msichana wa pekee na wa kwanza aliyewahi kupata daraja la kwanza katika masomo yake wakati akisoma katika shule ya sekondari Kituli iliyopo katika kijiji hicho tangu ianzishwe mwaka 1997, na alifaulu kujiunga na kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Nganza iliyopo jijini Mwanza na baadae kujiuga na Chuo kikuu cha Dodoma,” alisema Mbunge huyo.
Awali akiongoza ibada ya mazishi yaliyofanyika nyumbani kwao marehemu katika kijiji cha Kituli, Padre Emmanuel Makolo wa Parokia ya Busanda jimbo katoliki la Shinyanga alisema kifo cha ghafla cha kijana huyo msomi ni mipango ya mungu, hivyo kuwaomba wanafamilia na jamii kwa ujumla kuwa wavumilivu huku akiongeza kuwa hakuna haja ya kulaumiana kuhusu kifo hicho.
“Mungu hana upendeleo,nawaomba muishi kama hakuna kesho,jiandaeni kwa kifo kwani hakina muda wala eneo maalum,huku mkikumbuka kwamba kifo ni njia ya kila mwanadamu,” alisema Padre huyo.
Marehemu baada ya kuhitimu masomo yake alikwenda nyumbani kwao Kituli Julai 5 mwaka huu na Julai 13 alisafiri kwenda mkoani Geita kutafuta kazi katika mgodi wa madini wa Geita (GGM) na kufikia nyumbani kwa kaka yake anayeishi mkoani humo.
Akiwa kwa kaka yake siku iliyofuata 14 Julai ghafla alianguka na kuanza kutoa mapovu mdomoni kisha kukimbizwa hospitali ambapo muda mfupi baadae alifariki.