Na Mariam Kamgisha, MOROGORO
KAMATI ya maafa ya kijiji cha Magole wameilalamikia kamati ya maafa ya wilaya ya Kilosa kwa kushindwa kuwafikishia misaada wanayopewa waathirika wa mafuriko.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyetembelea kambi ya waathirika wa mafuriko iliyopo skuli ya sekondari Magole baadhi yaa wajumbe na waatrhirika hao walidai pamoja na kushuhudia misaada ikitolewa,bado hawapatiwi chakula cha kutosha na kwa wakati.
Walidai chakula wanachopewa ni kidogo na kisichotosheleza mahitaji, huku kingine wakishuhudia kikiondoka bila kuelezwa wala kujua ni wapi kinapopelekwa.
Mwenyekiti wa kamati ya maafa wa kijiji cha Magole, Ally Ngulungu, alisema mpaka sasa waathirika wanaishi katika hema moja watu wanane ukiondoa watoto.
Alisema waathirika wanaokaa kambini pekee ndio wanaopatiwa huduma ya chakula cha msaada,ambapo alidai waathirika waliohifadhiwa na jamaa,maraiki na ndugu hawapatiwi msaada wowote.
“Tangu kutokea kwa mafuriko mahema yaliyokuja kambini ni 24 tu leo ndio unaona hivi ujenzi wa mahema unafanyika ili kupunguza idadi ya watu katika hema moja,cha kushangaza zaidi ni kamati ya maafa ya wilaya kutotushirikisha sisi kamati ya kijiji,tunapata wasiwasi chakula na mahitaji mengine yanapokwenda,”alisema.
“Tangu maafa kutokea ni kilo 24.5 ndizo tulizopewa na hizo tunaambiwa ni kwa mwezi mmoja,hivi ndugu mwandishi kilo hizo kwa mwezi mzima zinatosheleza kweli,wakati tunasikia watu wengi wanatoa misaada,”alisema.
Waathirika wa mafuriko hayo Shabani Ndunda,Kigolo Abdallah na Idd Chidako, kwa nyakati tofauti waliitaka serikali kuwa na uazi wakati wa ugawaji wa misaada ili kuondoa hofu kwa waathirika.
Pamoja na kushukuru kwa misaada inayotolewa na wahisani,waliishauri serikali kuwasaidia ujenzi wa nyumba za kudumu, badala ya kuendelea na ujenzi wa mahema.
Akizungumzia madai yaliyotolewa na waathirika hao mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alisema misaada inayotolewa na wahisani inahifadhiwa katika ghala maalumu kwa maandishi na kutolewa kwa utaratibu kwenda kwa waathirika.
Aliwaondoa hofu Watanzania kuhusu misaada ya waathirika wa mafuriko kwa madai kuwa ugawaji wa chakula cha msaada umepangwa kwa kuzingatia wilaya zote tatu zilizoathiriwa na mafuriko.