Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, amewataka wakazi wa Handeni na maeneo inakopita barabara ya Mkata–Handeni na Korogwe–Handeni, kutumia ipasavyo fursa ya barabara hizo,kuboresha maisha yao .
Alitoa rai hiyo wakati wa sherehe za ufunguzi wa barabara inayounganisha makao makuu ya wilaya ya Handeni na barabara kuu ya Tanga-Dar es Salaam kupitia Mkata na upande mwingine kuunganisha na barabara kuu ya Tanga-Moshi- Arusha kwa upande wa Korogwe.
Alisema lengo la serikali ni kuona barabara ya Mkata hadi Handeni inaendelezwa hadi Kondoa kupitia Kiberashi kwani kufunguka kwa ukanda huo kutakuwa chachu ya kuinua uchumi.
Akiwasilisha tarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale, alisema barabara ya Mkata - Handeni ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami ina urefu wa kilometa 53.2 na imejengwa na Mkandarasi Sinohydro Corporation Ltd kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama ya shilingi bilioni 57.3.
Alisema mkataba wa mradi huo ulisainiwa mwezi Juni 2009 na kazi zikakamilika Novemba 2012 baada kutatua changamoto zilizokwamisha kukamilika kwa mradi huo mapema.
Ufunguzi wa barabara hiyo umeenda sambamba na ufunguzi wa barabara ya Korogwe hadi Handeni ambayo imekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.
Akitoa tarifa kuhusu miradi huo wa Korogwe- Handeni, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Patrick Mfugale, alisema mkandarasi Sinohydro Corporation Ltd ndiye pia iliyejenga barabara hiyo ambayo ina urefu wa kilometa 65.
Naye Waziri wa Ujenzi,Dk. John Pombe Magufuli, akielezea baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na kujengwa kwa barabara hizo alibainisha kuwa barabara ya kutokea Korogwe hadi Handeni ndiyo itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa gari katika barabara kuu ya TANZAM hasa kwa wasafiri na wasafirishaji wanaotokea maeneo ya Iringa, Mikumi na maeneo mengine ya ukanda huo.