Na Pascal Buyaga, MUSOMA
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimesema hakikubaliani na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa Dodoma wakati akizundua bunge maalum la katiba, kikisema hotuba hiyo imeligawa taifa.
Kauli hiyo imetolewa mjini Musoma na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Leticia Ghati Mosore, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema rais alipaswa kuzindua na kisha kuwaachia wajumbe waamue kile kilichowasilishwa na Tume ambayo aliiunda yeye, badala ya kupingana na tume hiyo.
Alisema kama anafikiria Tume haikufanya kazi vya kutosha, alipaswa aaite na kuwashauri wajumbe wake kabla ya kuiwasilisha.
“Tulisikitika kumuona Rais anatoa mapendekezo ya chama chake, wakati yeye ni alama ya taifa, kwa nini alikubali kupokea rasimu ya kwanza na rasimu ya pili wakati anajua ilikuwa na makosa kwa nini asingeshauriana na tume hiyo ambayo imepoteza mabilioni ya walipa kodi ya Watanzania,” alihoji.
Aidha alisema hotuba ya Kikwete imezungumzia kero za upande mmoja wa Zanzibar badala ya kuzungumzia keri za muungano.
“Sisi kama Watanzania tunamuomba Mungu awape busara wajumbe wa bunge la katiba, lakini kama NCCR-Mageuzi tunapinga hotuba yake,” alisema.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, alisema chama chake kimejipanga kuhakikisha kinachukua idadi kubwa ya mitaa.