Na Asya Hassan
JESHI la Polisi mkoa wa mjini magharibi Unguja, linamshilia Khamis Said Faki mkaazi wa Kwamtipura kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya Tatu Makame iliopo Kwamtipura wilaya ya mjini Unguja, baada ya kumtuhumu kuwa mwanga.
Kamanda wa Polisi mkoa huo, Kamishna Msaidizi,Mkadam Khamis Mkadam, alisema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Muembe Madema.
Alisema tukio hilo lilitokea Machi 22, baada ya mtuhumiwa akiwa na mwenzake kwenda nyumbani kwa mwanamke huyo kwa lengo la kuichoma moto nyumba yake.
Alisema walipofika waliimwagia mafuta ya petroli nyumba hiyo na kuanza kuichoma moto lakini hata hivyo, moto huo uliwahiwa kuzimwa kabla haujaleta athari kubwa.
Katika tukio jengine, raia wa Canada, alietambuliwa kwa jina la Christopher Bourvier Bouker (25) alishambuliwa kwa kuchomwa kisu cha chini ya kitovu akiwa katika matembezi Darajani.
Alisema mtuhumiwa alitambuliwa kwa jina la Takadir Khamis, ambae anasadikiwa kuwa na tatizo la ugonjwa wa akili.
Alisema majeruhi alikimbizwa hospitali ya Mnazimmoja kwa matibabu na kuruhusiwa baada ya hali yake kuendelea vizuri.