Na Masanja Mabula, PEMBA
KIKOSI maalumu cha kuzuia magendo (KMKM) kisiwani Pemba , kimekamata magunia 34 ya karafuu kavu ambazo zilikuwa katika harakati ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa njia ya magendo.
Kamanda wa KKMK kamandi ya Pemba, Silima Haji Haji, alisema karafuu hizo zimekamatwa katika bandari bubu ya Gome iliyoko Kinowe Micheweni usiku wa kuamkia Jumapili majira ya saa nane usiku.
Alisema karafuu hizo zimekamatwa na askari wa kikosi hicho kambi ya Msuka kwa kushirikiana na wale wa makao makuu ambao walikuwa katika doria zao za kawaida.
Alisisitiza haja kwa wananchi kuendelea kuuza karafuu zao katika vituo vya Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) ambalo limepewa jukumu na serikali la kununua karafuu na kujiepusha na biashara ya magendo.
Alisema wafanyabiashara wa magendo ya karafuu hawana nia njema na uchumi wa nchi kwani wanachojali ni maslahi yao binafsi na kuwataka wananchi kuepukana nao kwani wanaikosesha mapato serikali.
Hii ni mara ya tatu kwa kikosi hicho kisiwani hapa kuzima majaribio ya utoroshwaji wa karafuu kavu kwenda nje ya nchi kwa njia ya magendo ambapo kwa kipindi cha mwaka huu magunia 118 yamekamatwa.