Na Rehema Mohamed, PEMBA
MSHINDI wa shindano la bahati nasibu, lililoandaliwa na Kamisheni ya Utalii, Bi Agnes Barbra Tayari, amewataka wanajamii kuitumia dhana ya Utalii kwa wote, ili kuweza kutembelea sehemu za utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi kwenye hoteli ya Misali nje kidgo ya mji wa Chakechake, mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea maeneo kadhaa ya utalii na kihistoria kisiwani Pemba, alisema suala la kufanya utalii linwahusu pia wananchi wa kawaida.
Aliesema kuwa utalii kwa wote ni dhana ambayo inaweza kuwajengea uelewa wa sehemu za utalii, na kuweza kujifunza mengi ambayo yanaonekana katika sehemu hizo, ikiwemo maeneo ya kihistoria.
Alisema kuwa, utalii usichukuliwe kuwa ni sehemu ya kuvunja maadili, na kuwaona watu ambao wanafanya kazi sehemu za utalii, kuwa wamepotea bali ni sehemu muhimu ya kazi kama sehemu nyengine, kwani wanawajibika vizuri, tofauti na wanavyofikiria baadhi ya watu katika jamii.
Bi Agnes alisema kuwa, mashindano yanapowekwakatika jamii, ni vizuri kushiriki ili kuweza kujipatia nafasi muhimu za kujijengea uwezo, na kuweza kujiengezea uelewa wa sehemu za kitalii na kihistoria kwa ujumla.
Zanzibar imebahatika kupata sehemu nyingi za kitalii, ambazo zinaweza kutuingizia mapato ya nchi, na kuweza kuwajengea uzoefu watoto,ikiwa wataweza kutembelea maeneo hayo, kila baada ya kipindi na kuweza kuifahamu vizuri historia ya nchi hii.
“Iwapo tutazitumia vizuri fursa hizi, tunaweza kukuza viwango vya utalii wa ndani, kwani kuna baadhi ya watu wanaonakuwa, utalii ni unapaswa kufanywa na wageni tu, bali hata sisi tunauwezo wa kufanya hivyo, ilikuweza kutembelea maeneo hayo”, alisema.
“Nimefarijika kutembelea sehemu nyingi za utalii ikiwemo, Ufugaji wa popo, Ngezi, Vumawimbi, Chumba cha chini ya bahari, Sansity Beach iliopo Wesha, na nimefarijika sana kutokana na fursa hii niliyoipata kupitia Kamisheni ya Utalii”, alifahamisha Bi Agnes.
Nae Afisa Habari Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Amour Mtumwa Ali, alisema kuwa, mashindano hayo waliyaandaa kwa ngazi ya watoto na watuwazima, na wamepata washindi mbali mbali na kutembelea katika maeneo mbali mbali ya kitalii.
Alisema kuwa, kwa upande wa watoto, walishindanisha watoto kuanzia darasa la tatu hadi darasa la kumi na mbili na wulipata washindi 64, na wamewatembeza katika sehemu ya kitalii, ikiwemo mashamba ya viungo, Mjimkongwe, Jonzani na Zanzibar Paki Mwera.
Katika kulikamilisha hili na kuweza kuona kuwa dhana ya utalii kwa wote linakubaliwa na kuungwa mkono, sehemu za kitalii ikiwemo Hoteli ya jonzani na Zanzibar Pak, zimechukua juhudi za kuweza kuwadhamini washindi ambao wamepata fursa hii, ili kuweza kuwatia moyo jamii kufanya utalii katika visiwa vyetu vya Zanzibar.
“Mara baada ya kuwapata washindi katika shindano hilo, tuliwapeleka maeneo tuliyowaahidi, na katika kulikamilisha hilo wenzetu wa maeneo hayo ya utalii waliungana nasi, na kutusaidia gharama za usafiri, chakula na uingiaji wa sehemu za utalii”, alielezea Afisa habari Kamisheni ya Utalii.
Aidha, aliwataka wananchi kufanya utalii wa ndani, ili kuweza kujua maeneo mbali mbali, ambayo yanahistoria kubwa Zanzibar, na kuweza kuondokana na dhana kuwa, utalii unafanywa na wageni tu, wanaotoka nje ya nchi